Prof. George Msalya Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania akizungumza Leo Aprili 15,2025 Jijini Dodoma kwenye kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo.
Dkt. Charles Mhina Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) ina mpango wa kuanzisha maduka ya kisasa ya kuuza maziwa, yanayotarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Hatua hii inalenga kuchochea unywaji wa maziwa nchini huku ikitoa nafasi kwa wafugaji kuuza maziwa yao kwa uhakika wa soko, jambo linalotarajiwa kuongeza kipato chao na kukuza uchumi wa maeneo ya vijijini na mijini.
Mpango huo umetangazwa leo, Aprili 15, 2025 jijini Dodoma na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini, Prof. George Msalya, alipokuwa akizungumza katika kikao cha watumishi wa Bodi hiyo.
Amesema kuwa endapo mpango huo utatekelezwa ipasavyo, utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha lishe ya wananchi na kuchochea maendeleo ya sekta ya maziwa.
Prof. Msalya amefafanua kuwa maduka hayo – maarufu kama “bar za maziwa” – yatakuwa na bidhaa mbalimbali zitokanazo na maziwa kama vile maziwa ya kawaida, mtindi na bidhaa nyingine zilizosindikwa, huku kipaumbele kikiwa ni ubora na usalama wa bidhaa.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa awali utaanza kwa majaribio katika mikoa kadhaa kabla ya kuenea nchi nzima.
“Lengo letu ni kuvunja fikra potofu kuwa maziwa ni kwa watoto au wagonjwa pekee. Tunataka yawe sehemu ya maisha ya kila siku kwa watu wa rika zote,” amesema Prof. Msalya, akibainisha kuwa maduka hayo yataendeshwa katika mazingira rafiki, yenye huduma bora, na kuendeshwa na vijana waliopata mafunzo maalum kuhusu afya na usafi wa mazingira.
Aidha, TDB imejipanga kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika na afya na viwango ili kuhakikisha kila bidhaa inayouzwa kupitia maduka hayo inakidhi viwango vya usalama na ubora vinavyokubalika kitaifa. Elimu kwa umma kuhusu faida za lishe inayotokana na maziwa pia itatolewa sambamba na kampeni za uhamasishaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina, alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha watumishi wa bodi hiyo umuhimu wa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji, na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao. Alisisitiza kuwa maadili ya utumishi wa umma ni msingi muhimu wa mafanikio ya taasisi yoyote.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Riziki Shemdoe, Dkt. Mhina alieleza kuwa nidhamu ya ndani na utendaji wa kiwango cha juu kutoka kwa watumishi ndiyo itakayosaidia kufanikisha malengo makubwa ya bodi hiyo. “Tuwe mfano wa kuigwa kwa kutumia nafasi tulizonazo kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sekta ya maziwa,” alisema.
Aliongeza kuwa uwajibikaji binafsi wa kila mtumishi ni silaha muhimu ya kuongeza ufanisi wa taasisi kwa ujumla na kuchochea mabadiliko chanya katika sekta hiyo. Alihimiza pia umuhimu wa kuwa na ari ya kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na teknolojia mpya na mahitaji ya sasa ya soko la maziwa.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watumishi kupata mafunzo ya mara kwa mara, sambamba na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi, mamlaka za mikoa, na mashirika mengine ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi mikubwa kama huu unakuwa na mafanikio ya haraka.
Social Plugin