
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika Kinjolu kata ya Kikolo Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma Bosco Turuka kushoto,akikagua uzalishaji wa Kahawa katika moja la shamba la mkulima katika kijiji cha Kikolo ,wengine ni baadhi ya Wanachama wa Kinjolu Amcos.

Na Regina Ndumbaro-Mbinga.
Wakulima wa kahawa wanaohudumiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika Kinjolu Amcos kata ya Kikolo na Kihungu, Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma, wameiomba Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaonunua kahawa kwa magendo na wengine kununua kahawa ikiwa bado shambani.
Mwenyekiti wa chama hicho, Bosco Turuka, amesema kuwa kila msimu wa mavuno wafanyabiashara hao hupita mashambani na kuwarubuni wakulima kuuza kahawa kwa bei ndogo, huku wakitumia vipimo haramu vya magoma vinavyowanyonya wakulima na kuwakwamisha kiuchumi.
Amesema kuwa iwapo Serikali itadhibiti vitendo hivyo, wakulima wataongeza kipato na uzalishaji, hasa baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kuanzisha mpango wa utoaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima wa kahawa.
Kwa mujibu wa Turuka, mpango wa mbolea za ruzuku umeongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 93 msimu wa 2022/2023 hadi tani 192 msimu wa 2024/2025. Aidha, alisema kuwa ruzuku hiyo imeongeza kipato cha wakulima na kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba bora, kununua vyombo vya usafiri, na kusomesha watoto wao.
Pia, ruzuku hiyo imehamasisha wanachama wapya kujiunga na Ushirika kutoka wanachama 93 hadi 300.
Turuka amesema kuwa kutokana na usimamizi madhubuti wa Serikali kupitia mfumo wa stakabadhi gharani msimu wa 2024/2025, wakulima wameuza kahawa kwa bei nzuri ikilinganishwa na kama wangeruhusiwa kuuza kwa makampuni au watu binafsi, ambapo wangeambulia bei ya chini.
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kufanya matengenezo ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao, kwani ubovu wa miundombinu unatoa mwanya kwa walanguzi kununua mazao moja kwa moja mashambani kwa bei ya chini.
Kwa upande wake, mkulima Gotan Komba ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefufua na kuimarisha sekta ya ushirika, jambo lililowezesha wakulima kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa na mazao mengine.
Amesema kuwa hapo awali walikuwa wakilima bila kupata manufaa makubwa kutokana na gharama kubwa za uzalishaji, lakini mpango wa ruzuku ya mbolea umepunguza gharama hizo na kuhamasisha wakulima kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
Ameiomba Serikali kuendeleza mpango huo kwa kutoa pembejeo zaidi, hasa mbolea na dawa za kuua wadudu, ili kuongeza ufanisi katika kilimo cha kahawa ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma.
Hilda Komba, mkulima kutoka kijiji cha Kikolo, naye amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango na juhudi za wakulima wa kahawa.
Amesema utoaji wa ruzuku ya mbolea umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa kahawa.
Aidha, amempongeza Waziri wa Kilimo kwa kutoa bure miche bora ya kahawa kwa wakulima, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji, kuboresha maisha ya wakulima, kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Social Plugin