Na Dotto Kwilasa,DODOMA
Kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Boniphace Gisima Nyamo-Hanga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Gerson Msigwa amemtaja marehemu huyo kuwa alikuwa ni mtu muhimu kwa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Aprili 14,2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma, Msigwa amesema Nyamo-Hanga alikuwa mchapa kazi na mzalendo aliyejitolea mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini.
Msigwa amesema kifo hicho ni pigo kubwa siyo tu kwa TANESCO na familia, bali pia kwa nchi nzima iliyokuwa inaendelea kunufaika na uongozi wake imara na mawazo bunifu katika kuboresha huduma za umeme kwa Watanzania.
“Tumempoteza mtu mwenye maono makubwa,Eng. Nyamo-Hanga alikuwa miongoni mwa viongozi wachache waliokuwa na dira na uzalendo wa kweli katika kulitumikia taifa,alikuwa tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Idara ya Habari-Maelezo na kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ,aidha natoa pole kwa familia ya dereva wa Mkurugenzi kwa kumpoteza mtu mahiri,"amesema
Kutokana na hayo Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu na kutoa heshima zote stahiki kwa kiongozi huyo aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya taifa
Ikumbukwe kuwa ajali hiyo ya kusikitisha ilitokea usiku wa kuamkia Aprili 13, katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, ameeleza kuwa ajali hiyo ilitokea usiku baada ya gari walilokuwa wakisafiria marehemu na dereva wake kugongana uso kwa uso na lori, baada ya kumkwepa mwendesha baiskeli.
Wakati huo huo, viongozi mbalimbali wa serikali, wafanyakazi wa TANESCO na wananchi wameendelea kutuma salamu za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, wakimkumbuka marehemu kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme, ikiwemo ile ya ujenzi wa vituo vya kuzalisha na kusambaza nishati vijijini.
Marehemu Eng. Nyamo-Hanga alikuwa miongoni mwa wasomi wachache waliobobea katika taaluma ya uhandisi wa umeme, na alipanda ngazi serikalini kutokana na umahiri wake kazini, hadi kufikia nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO.
Alijulikana kwa kuhimiza uwajibikaji, uwazi, na matumizi sahihi ya rasilimali za shirika hilo muhimu kwa taifa.
Malunde Blog Media tunaungana na Watanzania wote katika kipindi hiki cha majonzi, na tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.
Social Plugin