
Mbunge wa Jimbo la Madaba Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama
Na Regina Ndumbaro-Arusha.
Mbunge wa Jimbo la Madaba na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dkt. Joseph Kizito Mhagama, ameshiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari yanayofanyika jijini Arusha.
Tukio hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari kwa lengo la kujadili maendeleo, changamoto na mustakabali wa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Mhagama ameeleza kwa kina namna ambavyo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kulinda uhuru wa habari.
Amebainisha kuwa mojawapo ya hatua muhimu ni kutungwa kwa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, pamoja na kufanya marekebisho ya sheria hiyo mwaka 2023 ili kuendana na mahitaji ya sasa ya tasnia hiyo muhimu.
Dkt. Mhagama amefafanua kuwa marekebisho hayo ya mwaka 2023 yanalenga kuinua viwango vya taaluma ya habari kwa kuwataka waandishi wote nchini kuhakikisha wanakuwa na angalau stashahada (Diploma) ya uandishi wa habari ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu sheria hiyo kufanyiwa marekebisho.
Hatua hii inalenga kuboresha weledi na maadili ya wanahabari sambamba na kulinda tasnia dhidi ya ukengeushi wa kitaaluma.
Aidha, Dkt. Mhagama amesisitiza kuwa sheria hii si adhabu bali ni fursa ya kuimarisha hadhi ya vyombo vya habari na kuondoa ukanjanja unaochafua taswira ya tasnia hiyo.
Amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya serikali, vyombo vya habari na taasisi za mafunzo ili kuhakikisha waandishi wanapata ujuzi na sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Social Plugin