
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa CWT kutoka Mkoa wa Ruvuma, Sabina Lipukila, na Mwenyekiti Kalemeje Sandali wakipongezana baada ya kutetea nafasi zao.


Katibu wa CWT Mkoa wa Ruvuma Rashid Mchekenje akimpokea Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Chacha aliyekuwa mgeni rasmi wa mkutano huo, katikati ni Mwenyekiti Kalemeje Sandali.

Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Ruvuma wakimsikiliza Katibu wa Chama hicho Rashid Mchekenje (hayupo pichani) akitoa taarifa mbalimbali za kipindi cha miaka mitano katika Ukumbi wa Sky Way, Wilaya ya Tunduru.

Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Ruvuma Kalemeje Sandali akizungumza na wawakilishi wa Walimu kutoka Wilaya tano za Mkoa huo, akiwa na Mweka Hazina Lenzile Mahena na Katibu wa Wanawake wa CWT Mkoa Lulu Njau
Na Regina Ndumbaro-Tunduru.
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Ruvuma kimeiomba Serikali kuangalia upya suala la kikokotoo cha mafao ya walimu kutoka asilimia 40 wanayopokea sasa hadi kufikia asilimia 50 ili kuongeza ari ya walimu katika kazi zao.
Maombi hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma, Kalemeje Sandali, alipokuwa akizungumza na wawakilishi wa walimu kutoka Wilaya tano za Mkoa wa Ruvuma katika Uchaguzi Mkuu wa kuwapata viongozi wa ngazi ya Mkoa uliofanyika katika Ukumbi wa Sky Way mjini Tunduru.
Amesema suala la kikokotoo limekuwa changamoto kubwa kwa walimu na kuiomba Serikali kuendelea kuboresha maslahi yao ili kwenda sambamba na kupanda kwa gharama za maisha.
Kalemeje ameeleza kuwa anaamini Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itasikiliza kilio hicho na kuchukua hatua stahiki.
Aidha, Kalemeje ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kutatua kero mbalimbali zinazowakabili walimu, ikiwemo kuboresha miundombinu ya elimu ambayo imeongeza ari ya kufanya kazi kwa walimu wengi.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, CWT Mkoa wa Ruvuma imeanzisha na kusimamia miradi mbalimbali ya kiuchumi kama vile ununuzi wa mabasi kwa ajili ya kurahisisha safari za walimu, hatua iliyoongeza ustawi wa chama na wanachama wake.
Katibu wa chama hicho, Rashid Mchekenje, amewataka walimu kufanya kazi kwa weledi, kufuata maadili ya kazi huku akisisitiza kuwa chama kitahakikisha shule zote za msingi, sekondari na taasisi za elimu zinatembelewa ili kusajili wanachama wapya, pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wastaafu.
Kwa mujibu wa Mchekenje, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, CWT Mkoa wa Ruvuma kimefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi 568,742,812.59 kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo marejesho ya asilimia 8 na mapato ya pango la jengo la chama.
Amesisitiza kuwa chama kitaendelea kusimamia na kufuatilia madai mbalimbali ya wanachama kama madaraja, posho, uhamisho na matibabu.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa CWT anayewakilisha Mkoa wa Ruvuma, Sabina Lipukila, ameahidi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha changamoto za walimu zinatatuliwa na mazingira bora ya kazi yanapatikana.
Amesisitiza umuhimu wa walimu kufanya kazi kwa bidii ili Mkoa wa Ruvuma uwe miongoni mwa mikoa inayoongoza kitaifa katika matokeo ya mitihani.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Simon Chacha, amekipongeza Chama cha Walimu Mkoa wa Ruvuma kwa kuendesha uchaguzi kwa mujibu wa Katiba yao inayotaka uchaguzi kufanyika kila baada ya miaka mitano.
Chacha ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa za kuboresha sekta ya elimu nchini, ikiwemo kuboresha miundombinu na mazingira ya kazi kwa walimu.
Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu, ikiwemo madai ya posho, ili kuongeza ari na ufanisi katika sekta ya elimu.
Social Plugin