
AZIMIO LA ARUSHA KWENYE KONGAMANO LA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI 2025 ARUSHA, TANZANIA
Sisi, Waandishi wa habari na Wadau wa Habari Tanzania tulioshiriki kwenye Mkutano wa Kitaifa kuadhimisha miaka 32 ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani uliofanyika kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 mwaka 2025 jijini Arusha, kwa pamoja tumeazimia kuwa tutaendelea kulinda na kutetea uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari kama msingi mkuu wa kutetea, kulinda na kukuza haki nyingine za msingi za binadamu nchini, ambazo kwa pamoja, huchangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki hizo na ushiriki wao katika mchakato wa maendeleo.
YAFUATAYO NI MAAZIMIO KWA WADAU MAALUM WA VYOMBO HABARI:
1.0 TAASISI ZA VYOMBO VYA HABARI NA WADAU
1.1 Kuwekeza zaidi katika teknolojia zinazoibuka na kutoa rasilimali za kifedha kwa vyombo vya habari ili kuweza kuendesha mafunzo ya ndani kwa waandishi wa habari kutoka vyombo vyenye mawanda mapana na redio za kijamii kuhusu sheria na kanuni za uchaguzi, na matumizi ya akili mnemba ili kukabiliana na taarifa zisizo za ukweli, taarifa za upotoshaji na taarifa za uzushi wakati wa uchaguzi mkuu.
1.2 Kuongeza ushirikiano kwa kuwekeza katika mifumo ya kidijitali na taarifa, pamoja na tafiti ili kuhakikisha utungwaji kwa sheria ya kikanda ili kudhibiti na kulinda uhamishwaji wa taarifa na kukabiliana na teknolojia hatarishi.
1.3 Kusaidia vyombo vya habari kulea, kufundisha na kuwaongoza kuhusu uandishi unaozingatia usawa wa kijinsia na kuunda mazingira rafiki na salama kwa waandishi wa habari na wanasiasa wanawake katika ulimwengu wa kidijitali.
1.4 Kufuatilia viashiria vya kauli za chuki, upotoshaji na kuweka mikakati ya kukabiliana nayo.
1.5 Kuanzisha viwango vya kitaifa juu ya maadili ili kudhibiti maudhui yaliyotengenezwa kwa kutumia akili mnemba katika vyumba vya habari.
1.6 Mamlaka, taasisi na vyama vya siasa viheshimu na kulinda Uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha hakuna vitisho, ushawishi wa kisiasa au vikwazo vinavyowekwa kwa wale wanaohakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi.
2.0 VYOMBO VYA HABARI
2.1 Kuwapatia waandishi wa habari mikataba ya ajira na kuwalipa malipo stahiki ili kuboresha weledi wao.
2.2 Kupokea na kuwekeza katika teknolojia ya akili mnemba na kidijitali, simulizi zenye maslahi kwa umma pamoja na kutoa mafunzo ya ndani kwa waandishi wa habari ili kuongeza elimu ya kidijitali.
2.3 Kuwalinda waandishi wa habari na wanasiasa wanawake dhidi ya ukatili wa kimwili na wa mitandaoni na kuwapatia msaada wa kitabibu na kisaikolojia kwa manusura.
2.4 META wafungue ofisi zao nchini Tanzania ili kuwasogezea huduma Watanzania ambao ni waandaaji wa maudhui ya kidijitali.
3.0 WAANDISHI WA HABARI
3.1 Wazingatie maadili na kukubali kujisimamia, ili wasipoteze imani kwa umma, kuzuia mgawanyiko katika jamii, taarifa za uzushi, upotoshaji na uongo.
3.2 Kujifunza teknolojia mpya kama akili mnemba, kuripoti habari kutoka maeneo ya vijijini na yasiyofikika kwa urahisi na kuhakiki taarifa kabla ya kuzichapisha.
3.3 Wanapaswa kuweka wazi maslahi yao endapo wanakusudia kugombea nafasi za kisiasa na wajiepushe kuripoti wakati wa uchaguzi, huku wakidumisha msimamo wa kutofungamana na upande wowote wa kisiasa.
3.4 Kupaza sauti kwa haki na usawa kwa makundi yote katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi na kutumia lugha rafiki zinazozingatia jinsia na watu wenye ulemavu.
3.5 Lazima washiriki kikamilifu katika kufichua na kuripoti pale uhuru wa vyombo vya habari unapoathiriwa kisiasa ili kuimarisha uwajibikaji wa umma.
3.6 Wanapaswa kutumia zana za akili mnemba kuwezesha uhariri wa haraka, sahihi na wa ufanisi zaidi hasa katika kipindi cha uchaguzi.
4.0 SERIKALI:
4.1 Lazima itengeneze mazingira wezeshi kwa ajili ya sera na kanuni za vyombo vya habari ambazo zinajumuisha wadau wote na kusikiliza maoni ya wananchi ili kupambana na teknolojia hatarishi.
4.2 Kusimamia mazingira ya kazi ya waandishi wa habari ili kuhakikisha wanafanya kazi bila hofu au vitisho.
4.3 Kusimamia vyombo vya dola viweze kuwatambua na kulinda waandishi wa habari kama wadau muhimu na kushughulikia ukatili wa mtandaoni na wa kimwili dhidi ya waandishi wa habari na wanasiasa wanawake katika michakato ya uchaguzi.
4.4 Kuchunguza na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa wanaohusika na ukiukwaji wa haki za waandishi wa habari.
4.5 Kusaidia mabadiliko ya sheria ili kuongeza uhuru wa vyombo vya habari na kuhalalisha kazi za kiuandishi
4.6 Dira ya Maendeleo 2050 inayotarajiwa kuzinduliwa, ijumuishe maoni na mitazamo ya watoto kuhusu Tanzania wanayoitamani.
5.0 VYAMA VYA SIASA:
5.1 Havipaswi kuingilia uhuru wa kiuhariri wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi mkuu.
5.2 Vinapaswa kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unakuwa jumuishi kwa makundi yote kuanzia uteuzi hadi uchaguzi wenyewe.



Social Plugin