Na Regina Ndumbaro-Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini mkoani Lindi, Mheshimiwa Ally Saleh Ndulane, ameungana na viongozi wengine kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio makubwa katika sekta ya nishati, amesisitiza kuwa jitihada hizo zimeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa maeneo ya vijijini na mijini.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Aprili 29,2025, Mheshimiwa Ndulane amesema kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya nishati ni uthibitisho wa dhamira ya serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanawafikia wananchi wote kwa usawa, hasa kupitia miradi ya kusambaza umeme hadi maeneo ya pembezoni.
Mbunge huyo ameeleza kuwa miradi kama ya kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP), pamoja na miradi ya nishati jadidifu ikiwemo ya Malagarasi, Kakono na Kishapu, ni vielelezo halisi vya dhamira ya serikali chini ya Rais Samia ya kukuza uchumi wa taifa na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Ndulane pia ameongeza kwa kuwapongeza Naibu Waziri Mkuu na Naibu Waziri wa nishati Mheshimiwa Judith Kapinga kwa kazi nzuri wanazonifanya kuhakikisha sekta ya umeme inakwenda vizur kwa Wananchi wote wanapata huduma safi ya umeme.
Mhe. Ndulane amesema mafanikio haya si tu yanachochea ustawi wa sekta ya viwanda na biashara, bali pia yanafungua fursa kwa wananchi wa maeneo kama Kilwa Kaskazini kuunganishwa kwenye mfumo wa nishati wa taifa, hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kasi zaidi.
Social Plugin