Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AIRTEL TANZANIA YAZINDUA KAMPENI YA 'AIRTEL SPAM ALERT-KATAA MATAPELI' KUPAMBANA NA UTAPELI WA SIMU



Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, akizungumza katika uzinduzi wa huduma maalum ya kutoa taarifa kuhusu utapeli kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba, uliofanyika leo Aprili 28, 2025, jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Kampuni ya Airtel Tanzania imezindua huduma maalum ya kutoa taarifa kuhusu utapeli kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba, iliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kuwaonya wateja dhidi ya ulaghai wa simu.

Huduma hiyo, Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli, inatumia teknolojia ya kisasa ya Akili Mnemba (AI) na inalenga kuimarisha juhudi za kupambana na matapeli wa simu nchini Tanzania.

Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli itapatikana kwa wateja wote wa Airtel, bila kujali aina ya simu wanayotumia, bila hitaji la kupakua programu au kuchukua hatua maalum. 

Wateja watapokea taarifa za haraka kuhusu jumbe zinazotiliwa shaka kuwa za kitapeli, hatua itakayosaidia kuwaepusha dhidi ya udanganyifu wa simu.

 Hii ni hatua muhimu katika kuongeza usalama wa mawasiliano na kuelimisha jamii kuhusu hatari ya utapeli.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, ameipongeza Airtel kwa ubunifu huo wa kiteknolojia unaosaidia kupambana na utapeli wa simu, akisema kuwa huduma hii inaunga mkono jitihada za serikali kutatua changamoto hiyo. 

Waziri Silaa amesema, "Huduma ya Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli inayotumia Akili Bandia kugundua ulaghai mtandaoni inaendana moja kwa moja na juhudi za serikali kulinda wananchi dhidi ya matapeli wa simu kwa haraka."

Ameongeza kuwa huduma hiyo inachangia katika kampeni ya kitaifa ya #Sitapeliki, inayolenga kuelimisha umma kuhusu udanganyifu wa simu na kuwawezesha wananchi kujikinga na matapeli.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, ameelezea umuhimu wa huduma hiyo kwa wateja wa simu janja na za kawaida. 

Kamoto amesema, "Hii si tu uzinduzi wa teknolojia mpya, bali ni tamko kuwa Airtel Tanzania ni mtandao wako wa kidijitali na mlezi wako. Tumejitoa kikamilifu kuwawezesha wateja wetu kuwa makini na kuwa na imani katika mawasiliano ya kidijitali."

Kamoto amehamasisha wadau wa sekta ya mawasiliano kuunga mkono mapambano dhidi ya utapeli wa simu na kuelimisha jamii kuhusu madhara ya udanganyifu. 

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya mawasiliano, serikali na jamii katika kuhakikisha usalama wa wateja na kupunguza vitendo vya utapeli.

Huduma ya Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli ni hatua kubwa katika kulinda wateja wa Airtel, na inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza matukio ya utapeli wa simu nchini Tanzania. 

Airtel itaendelea kuboresha huduma zake ili kuwapa wateja uzoefu bora na salama wa mawasiliano ya kidijitali, huku ikichangia katika mapambano dhidi ya udanganyifu.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, akizindua huduma huduma maalum ya kutoa taarifa kuhusu utapeli kupitia teknolojia ya Akili Mnemba, uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Aprili 28, 2025.
Baadhi ya wadau mbalimbali wa mawasiliano waliohudhuria uzinduzi wa huduma huduma maalum ya kutoa taarifa kuhusu utapeli kupitia teknolojia ya Akili Mnemba jijini Dar es Salaam leo Aprili 28, 2025.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com