
Mwenyekiti Wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akizungumza na Wananchi wa kata Ya Kilagano

Wananchi waliojitokeza kumsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho pichani hayupo katika ziara aliyoifanya kata ya Kilagano

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho


Na Regina Ndumbaro-Kilagano Songea.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, ameendelea na ziara yake katika Kata ya Kilagano, wilayani Songea Vijijini.
Ziara hiyo imelenga kuzungumza na wananchi wa vijiji vya Mgazini na Lugagala, ambapo amewapongeza kwa ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi wa vitongoji vyote kumi na mbili.
Amesema ushindi huo ni ishara ya imani kubwa waliyonayo wananchi kwa chama hicho na uongozi wake.
Katika mkutano wake na wananchi, Mwenyekiti Oddo Mwisho ametoa fursa ya maswali kwa wananchi kuhusu changamoto zinazowakabili.
Moja ya changamoto kubwa iliyobainika ni mgogoro wa Mlima wa Lihanje, ambao wananchi wa vijiji hivyo wameiomba serikali kuutatua kwa haraka.
Wananchi hao wamelalamika kuwa mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa suluhisho, hali ambayo imekuwa kikwazo kwa maendeleo yao.
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa ameeleza kuwa serikali inatambua changamoto hiyo na kwamba inafanya jitihada kuhakikisha inapatikana suluhisho la kudumu.
Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kuwa na subira huku serikali ikishughulikia suala hilo kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.
Pia amesisitiza kuwa viongozi wa serikali wanapaswa kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa ilani ya CCM ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote.
Katika ziara hiyo, Oddo Mwisho pia amegusia changamoto nyingine zinazowakabili wananchi wa Kata ya Kilagano, ikiwemo ukosefu wa umeme katika Shule ya Sekondari Mtopesi.
Amesema serikali ina wajibu wa kuboresha miundombinu muhimu kama umeme, maji, barabara, afya na elimu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo endelevu.
Aidha, Mwenyekiti huyo amewahimiza wananchi wa vijiji vya Mgazini na Lugagala kushirikiana na viongozi wa serikali na chama ili kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa kwa haraka.
Amewataka kushirikiana katika miradi ya maendeleo kwa manufaa ya jamii nzima na kuendelea kudumisha mshikamano katika chama na serikali yao.
Katika hotuba yake, Oddo Mwisho amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake imara na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Pia, amepongeza uteuzi wa Dkt. Emanuel Nchimbi na Dkt. Hassan Mwinyi kuwa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM.
Amesema uteuzi wa Dkt. Nchimbi ni heshima kubwa kwa Mkoa wa Ruvuma, hivyo wananchi wanapaswa kujivunia tunu hiyo na kuendelea kumuunga mkono.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Kilagano, akiwemo Christina Nguwo na Francis Mapunda, wameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi.
Pia wamemshukuru Mbunge wa Songea Vijijini na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, kwa juhudi zake katika kuwaletea maendeleo.
Wamempongeza pia Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Oddo Mwisho, kwa kuwatembelea na kusikiliza changamoto walizokuwa nazo kwa zaidi ya miaka thelathini, wakiamini kuwa hatua hiyo italeta suluhisho la kudumu kwa matatizo yao.
Social Plugin