Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKRISTO KAGERA KUNUFAIKA NA DARASA LA UJASIRIAMALI


Sehemu ya Darasa la ujasiriamali
Mwezeshaji wa mafunzo ya ujasiriamali Timotheo Mpendakazi kutoka kampuni ya Christ Enterpreneurship society akitoa elimu



Na Lydia Lugakila - Bukoba

Kampuni ya Christ Enterpreneurship society kutoka Mkoa wa Njombe imetoa mafunzo kwa Wananchi Mkoani Kagera hasa Wakrito kutoka madhehebu mbalimbali wakiwemo wa kanisa la Moravian lililopo katika Kijiji cha  Kagondo Karuguru kata ya kagondo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera lengo likiwa ni kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu mbali mbali za kuwainua ki uchumi.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoanza Februari 17,2025 mwezeshaji kutoka Mkoani Njombe Timotheo Mpendakazi amesema kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuwainua watu wengi hasa Wakrito katika kujikwamua kiuchumi ili wawe na mbinu mbali mbali za kiutafutaji bila kutegemea shughuli moja.

"Nimefika Kagera tangu Novemba, 2024 bado naendesha mafunzo matokeo ni mazuri Walengwa wameanza kuelewa wanachojifunza hasa utengeneza wa mafuta ya kujipaka pamoja utengenezaji wa sabuni mche "amesema Mpendakazi.

Mpendakazi Amesema kuwa atahakikisha Watanzania walio wengi hasa wenye kipato cha chini wanafikiwa na mafunzo hayo ili wajitegemee huku akiahidi kuzungukia makanisa 100 hapa Nchini kutoa elimu hiyo.

Amewaomba watu wa rika zote kuchangamkia fursa hiyo inayotolewa bure ili wapate maarifa yatakayowasaidia kwa baadae.

Mwezeshaji huyo ameyataja mafunzo anayofundisha kuwa ni pamoja utengenezaji wa viatu  vya shanga vya kike, kutotoresha mayai ya kienyeji bila kutumia mashine, kutengeneza dawa za matibabu ya kuku zisizokuwa na kemikali, utengenezaji wa mbolea ya kupandia na kukuzia isiyo na kemikali, kilimo cha bustani, namna ya kutunza pesa na mengineyo.

Amewaomba Watanzania kutokukosa maarifa hayo kwani ujuzi hauzeeki.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yameanza Februari 17, 2025 na yatatamatika Februari 22 Mwaka huu.

Aidha kwa upande wao Mery Stanslaus, Benson Mwamkinga kutoka Manispaa ya Bukoba wamesema kuwa mafunzo hayo  watayatumia vyema ili yawanufaishe wao pamoja na vizazi vijavyo.

Kwa upande wake mchungaji wa Kanisa la Moravian Jimbo la ziwa Tanganyika kata ya kagondo Manispaa ya Bukoba Peter Mayengo amesema kanisa hilo limechukua hatua kuhalika mwezeshaji huyo ili kuwaongezea ujuzi huku akiwataka Wananchi Mkoani Kagera kuchangamkia fursa hiyo ya mafunzo 12 bure.

Aidha mchungaji Mayengo amewataka Wananchi kuchangamkia fursa mbali mbali zinapotokea  bila kufungwa na itikadi zao waendelee kujifunza ujasiliamali kwani hakuna elimu iliyo ndogo huku wakitambua kuwa wakipata uelewa utawasaidia.

Mtumishi huyo wa Mungu amewashauri wataalam mbali mbali kutokaa na utaalam wao kwa kujifungia nao bali wawasaidie wanaousaka ujuzi ili wanufaike kwa pamoja na kujiletea kipato.

Hata hivyo ameishukuru kampuni ya Christ Enterpreneurship sociaty kwa namna ilivyoleta mafunzo hayo kwa ajili ya kuwanufaisha Wananchi hasa Wakrito Mkoani Kagera.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com