
Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Tanesco, Allan Njiro,
Na Regina Ndumbaro Malunde 1Blog-Songea.
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoani Ruvuma limeendelea kuboresha huduma ya umeme katika mtaa wa Pachanne B, kata ya Mjimwema.
Hatua hii imelenga kukabiliana na changamoto za awali zilizokuwa zikiwakumba wakazi wa eneo hilo.
Awali, mtaa wa Pachanne B ulikuwa ukikabiliwa na changamoto kubwa ya umeme, kutokana na transfoma moja pekee iliyokuwa ikihudumia matumizi ya viwanda na majumbani. Hali hii ilisababisha huduma duni na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, wananchi walilalamikia tatizo la umeme hafifu, jambo ambalo lilikuwa likikwamisha shughuli zao za kila siku, ikiwemo uzalishaji viwandani na matumizi ya nyumbani.
Ili kutatua tatizo hilo, Tanesco imeongeza transfoma nyingine, hivyo sasa eneo hilo litakuwa na jumla ya transfoma mbili.
Hatua hii itahakikisha mgawanyo bora wa umeme kati ya viwanda na matumizi ya majumbani, na hivyo kuboresha huduma kwa wakazi wa mtaa huo.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Tanesco, Allan Njiro, amefafanua kuwa mabadiliko haya yanalenga kuondoa kabisa kero ya umeme kuwa na nguvu hafifu.
Alisisitiza kuwa shirika hilo limejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata umeme wa kutosha kwa matumizi mbalimbali.
Mchakato wa uboreshaji wa miundombinu ya umeme umepata msaada mkubwa kutoka kwa Mama cha Urembo, ambaye alikubali kutoa eneo lake kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa mradi huo. Jitihada zake zimepongezwa na viongozi na wananchi wa eneo hilo.
Mwananchi wa mtaa wa Pachanne B, Saimon Gabriel Ndewele, amewashukuru viongozi wa Tanesco kwa kujali mahitaji ya wananchi na kupongeza jitihada za Mama cha Urembo kwa moyo wake wa kujitolea kusaidia maendeleo ya jamii.
Diwani wa kata ya Mjimwema, Silvester Mhagama, amesifu juhudi za Tanesco na kueleza kuwa hatua hii itasaidia kuongeza uzalishaji viwandani na kuboresha uchumi wa eneo hilo.
Pia ametoa pongezi kwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuboresha huduma za umeme na maendeleo ya miundombinu kwa wananchi.




Social Plugin