Na Dotto Kwilasa, KILIMANJARO
Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni, amewataka watumishi wa umma wilayani humo kuzingatia haki za binadamu wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na stahiki.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya Uraia na Utawala Bora, yaliyofanyika wilayani Same na kuendeshwa na Wizara ya Katiba na Sheria, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha utendaji kazi na utawala bora katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza katika kwenye mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya, Kasilda Mgeni, amesisitiza kuwa haki za binadamu ni muhimu katika utumishi wa umma, na kwamba watumishi wa umma wanapaswa kuwa waadilifu, watenda haki, na kuwajibika kwa wakati.
Mgeni amesema, "Naomba niwaahidi kuwa watumishi wangu, ni waaminifu na wataenda kutekeleza majukumu yao kulingana na mafunzo waliyoyapata kupitia Wizara ya Katiba na Sheria," amesema
Pia, Mgeni ameeleza kuwa kwa ngazi ya Wilaya, wataendelea kufuata kanuni za maadili, ikiwa ni pamoja na suala la mavazi ya ofisini, ili kuhakikisha kuwa utumishi wa umma unakuwa mfano wa ufanisi, heshima, na utawala bora.
Kwa upande mwingine, Mratibu wa mafunzo hayo, Prosper Kisinini, ameeleza umuhimu wa watendaji wa umma kusimamia vizuri miradi ya maendeleo, ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kuwaathiri wananchi.
Social Plugin