Zahanati ya Hanga Ngadinda iliyojengwa kwa juhudi za Mbunge wa Jimbo la Madaba mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama
Kibao cha Zahanati ya Hanga Ngadinda iliyojengwa na Mbunge Mhagama
Na Regina Ndumbaro Malunde 1 blog - Madaba.
Mbunge wa Jimbo la Madaba, Mhe. Joseph Kizito Mhagama, ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya ndani ya Kata ya Mtyangimbole, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma kwa wananchi.
Moja ya mafanikio hayo ni ujenzi wa Kituo cha Afya ambacho kinafanana na hospitali, hatua iliyolenga kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma za afya, hasa baada ya wananchi kutegemea Zahanati ya Misheni kwa miaka mingi.
Akizungumza katika ziara yake ya kikazi ya kutathmini utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka minne, pamoja na kupokea changamoto kutoka kwa wananchi wa vijiji mbalimbali ndani ya jimbo hilo, Mhagama amesisitiza kuwa maendeleo yaliyofanikishwa yanaonekana kwa macho.
"Mtu yeyote atakayesema mbunge hajafanya kitu, mbebe kwenye bodaboda aje aone maendeleo yaliyofanyika.
Tumejenga kituo cha afya katika eneo ambalo tangu nchi ilipopata uhuru hakijawahi kuwa nacho," alisema Mhagama kwa msisitizo.
Aidha, Mbunge huyo ameishukuru Kanisa Katoliki kwa mchango wake mkubwa katika kutoa huduma za afya kwa jamii ya eneo hilo kwa miaka mingi, kabla ya serikali kuweza kujenga kituo hicho kipya cha afya.
Mhagama amebainisha kuwa, kwa kushirikiana na Diwani wa kata hiyo na viongozi wengine, wamefanya ziara za ukaguzi wa miundombinu ya afya na kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Ameahidi kushughulikia changamoto hizo kwa wakati, ikiwemo ujenzi wa wodi mpya kwenye kituo hicho cha afya ili kuboresha zaidi huduma kwa wananchi.
Baadhi ya akina mama waliokuwepo katika eneo hilo wamempongeza Mbunge huyo kwa kutambua changamoto zao, hasa katika huduma za mama na mtoto.
Wamesema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha afya umesaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, huku ukiwarahisishia gharama za kusafiri umbali mrefu kwenda mijini kutafuta huduma bora, ambazo sasa wanazipata moja kwa moja katika kata yao.
Mradi huo ni moja ya mafanikio makubwa ya serikali katika kuboresha sekta ya afya ndani ya Jimbo la Madaba, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa ukaribu zaidi.
Social Plugin