
Na Regina Ndumbaro Malunde 1 blog - Songea.
Mbunge wa Jimbo la Madaba, Joseph Kizito Mhagama, amewataka wakazi wa Kijiji cha Ngadinda, Kata ya Gumbiro, Halmashauri ya Madaba kuwa na subira wakati mradi wa maji safi na salama ukiendelea kukamilika.
Mradi huo unatarajiwa kuanza kutoa huduma kwa wananchi hivi karibuni, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake ya kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wa kijiji hicho.
Akizungumza katika ziara yake ya kuelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM, Mhagama amesema kuwa mradi huo uko katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Aidha, ameeleza kuwa ndani ya kipindi cha wiki mbili, kazi ya kuchimba mitaro na kufukia mabomba itaanza, hatua inayosogeza mbele utekelezaji wa mradi huo.
"Mradi huu umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 1.3 na upo katika hatua nzuri. Tunawaomba wananchi waendelee kuwa na subira wakati ujenzi ukiendelea, kwa kuwa tunalenga kuwapatia huduma ya maji safi na salama kwa maendeleo ya jamii",amesema Mhagama.
Mbunge huyo pia amekiri changamoto wanazokabiliana nazo akina mama katika kutafuta maji na amewaahidi wakazi wa Kibaoni kwamba hivi karibuni kisima kirefu kitachimbwa ili kusaidia upatikanaji wa maji kwa shughuli za kilimo, hususan uzalishaji wa mboga mboga.
Kwa upande wake, Katibu wa Kata ya Gumbiro, Denis Innocent, ameipongeza Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kufanikisha mradi huo mkubwa.
Amesema kuwa kukamilika kwake kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa kijiji hicho.
Mradi huo wa maji ni hatua muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi wa Madaba na unatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji katika Kijiji cha Ngadinda.
Social Plugin