Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI RUVUMA WATAKIWA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA


Wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Mbinga na Nyasa wakiwa katika matembezi ya hiari jana kuunga mkono Azimio la Mkutano wa Chama hicho kwa kuwapitisha Rais Samia Suluhu kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hassan na Dkt. Hussen Ali Mwinyi kugombea Urais wa Zanzibar


Na Regina Ndumbaro Mbinga.

Wananchi wa mkoa wa Ruvuma wametakiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha yao. 

Wito huo umetolewa Januari 1,2025 na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya za Mbinga na Nyasa katika mkutano maalum wa kuunga mkono azimio la CCM la kuwapitisha Rais Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.


Mwisho ameeleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, maendeleo makubwa yamepatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara za lami, hospitali, zahanati, vituo vya afya, miradi ya maji, pamoja na vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari. 


Amesisitiza kuwa maendeleo haya yamechangia kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwaondolea kero ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za msingi.


Mwisho amewataka wapinzani wa kisiasa kutafuta maeneo mengine ya kufanya siasa kwa kuwa mkoa wa Ruvuma ni ngome imara ya CCM.


 Amesisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kuongoza dola kwa sababu kimefanikiwa kusimamia na kutekeleza ilani yake kwa vitendo. 


Ameongeza kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM itahakikisha inapendekeza wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge wenye sifa stahiki, huku akiwataka wanachama wake kuwakataa watu wanaotafuta uongozi kwa njia za rushwa.



Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kisare Makori, amesema katika kipindi cha miaka minne, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa zaidi ya shilingi bilioni 16.9 kwa ajili ya miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo. 


Aidha kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji safi na salama katika mji wa Mbinga, ili kuhakikisha asilimia 85 ya wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika.


Kuhusu sekta ya afya, Makori amesema kuwa serikali inaendelea na maboresho makubwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mbinga (Mbuyula) kwa kujenga majengo matatu mapya yatakayogharimu shilingi milioni 900. 


Vilevile katika sekta ya elimu, halmashauri ya wilaya ya Mbinga imepokea shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari tatu, huku halmashauri ya mji wa Mbinga nayo ikipokea kiasi kama hicho kwa ujenzi wa shule mpya.


Mbali na miradi hiyo, Makori amebainisha kuwa Halmashauri ya Mji Mbinga imeanza mchakato wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi katika eneo la Lusaka pamoja na kufanya maboresho makubwa katika soko kuu la Mbinga. 


Vilevile, Serikali imetenga shilingi bilioni 4.6 kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo.


Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa zaidi ya shilingi bilioni 25 kwa ajili ya kutekeleza miradi tisa ya maji wilayani humo. 


Ameeleza miradi hiyo imewezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa maji kutoka asilimia 65 hadi 75, huku katika mji wa Mbambabay huduma hiyo ikitarajiwa kufikia asilimia 80 baada ya kukamilika kwa miradi inayoendelea.


Magiri amesema miradi mingine muhimu inayoendelea kutekelezwa wilayani Nyasa ni ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mbaha na uboreshaji wa Bandari ya Mbambabay, ambapo Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 83 kwa ajili ya miradi hiyo. 


Amesema kuwa uwekezaji huu ni hatua muhimu katika kuifungua wilaya hiyo, ambayo hapo awali ilikuwa kama kisiwa kutokana na changamoto za miundombinu.


Kwa ujumla, viongozi hao amesisitiza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mkoa wa Ruvuma ni matokeo ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake katika kuboresha maisha ya wananchi. 


Hivyo, wamewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya CCM ili miradi hii iweze kuleta manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com