Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADIWANI MASASI WAPITISHA RASIMU YA BAJETI YA FEDHA BILIONI 47.85 MWAKA WA FEDHA 2025/2026

Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauter  J. Kanoni akizungumza na Madiwani wilayani Masasi


Na Regina Ndumbaro, Masasi

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, limepitisha rasimu ya Mpango na Bajeti ya Tsh 47,850,929,593 kwa mwaka wa fedha 2025/2026. 


Bajeti hiyo ina ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita, huku mapato ya ndani yakitarajiwa kukua kwa asilimia 16.8. 

Ongezeko hili linalenga kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi katika wilaya hiyo.

Afisa Mipango na Uratibu wa Halmashauri Ndg. Phabian Kabambara amewasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.


 Katika mawasilisho yake, amebainisha kuwa bajeti hiyo imezingatia miradi ya kimkakati yenye lengo la kuongeza mapato ya halmashauri na kuboresha maisha ya wananchi.


Miongoni mwa vipaumbele vya bajeti hiyo ni ujenzi wa ghala la mazao mchanganyiko katika kata za Chigugu na Chiungutwa. 


Ghala hili linalenga kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno. 

Aidha, halmashauri imepanga kununua lori moja kwa ajili ya kusafirisha vifaa na malighafi za miradi ya maendeleo ili kurahisisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika sekta ya mawasiliano na jamii, bajeti hiyo imeweka mkakati wa kuanzisha Redio ya Jamii ya Masasi. 

Lengo la redio hii ni kuongeza uhamasishaji wa wananchi juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo, afya, elimu, na usalama. Redio hiyo pia itawapa wananchi fursa ya kushiriki mijadala ya kijamii na kutoa maoni yao kuhusu uendeshaji wa halmashauri.


Kwa upande wa ulinzi na usalama bajeti hiyo imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya polisi katika kata za Chiwale na Mbuyuni.


 Vituo hivi vitasaidia kupunguza matukio ya uhalifu na kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao. Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauter J. Kanoni, ameliomba baraza la madiwani kuhakikisha linajenga kituo kidogo cha polisi katika makao makuu ya halmashauri yaliyopo Mbuyuni ili kuimarisha usalama katika eneo hilo.


Katika sekta ya afya, halmashauri imepanga kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya viwili katika vijiji vya Chikundi na Chikoropola pamoja na zahanati mbili katika vijiji vya Mbangala na Liloya. Uwekezaji huu unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa wananchi wa vijijini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hizo kwa karibu.

Sekta ya elimu pia imepewa kipaumbele katika bajeti hiyo, ambapo halmashauri imepanga kukamilisha ujenzi wa vyumba 56 vya madarasa, nyumba tatu za walimu, na vyumba vinne vya maabara. Hatua hii inalenga kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuhakikisha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.

Ili kukabiliana na uhaba wa watumishi wa umma bajeti hiyo imepanga kuajiri watumishi wapya 604 katika sekta mbalimbali. 

Kati yao watumishi 175 watapelekwa katika sekta ya afya, 214 katika elimu ya msingi, 76 katika elimu ya sekondari, huku kada zingine kama kilimo, mifugo, uhasibu, ujenzi, na utawala pia zikipata watumishi wapya. 

Ajira hizi zitasaidia kupunguza pengo lililosababishwa na kuongezeka kwa vituo vya huduma pamoja na kustaafu kwa baadhi ya watumishi wa umma.

Kwa ujumla  bajeti hii inalenga kuimarisha maendeleo ya Wilaya ya Masasi kupitia uwekezaji katika miradi ya kimkakati na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. 

Baraza la madiwani limeahidi kusimamia utekelezaji wa bajeti hiyo kwa umakini ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi na manufaa ya wananchi wote wa Masasi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com