Mhandisi wa tume ya Taifa ya Umwagiliaji Lucy Chaula kushoto na kulia kwake mkandarasi Mubaraka Ng’wada wakisaini mkataba wa mradi wa visima vya umwagiliaji katika kata ya Subira iliyopo Manispaa ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma
Mkandarasi Mubaraka Ng’wada akitoa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa ushirikiano na wananchi wa kata ya Subira kushirikiana katika mradi wa uchimbaji wa visima vya umwagiliaji
Mkandarasi Mubaraka Ng’wada akikabidhiwa Mkataba wa uchimbaji wa visima vya maji na Mkuu wa Mkoa Kanali Abbas Ahmed Abbas
Mwenyekiti Wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho Akizungumza na Wananchi wa kata ya Subira katika utiaji wa saini wa mkandarasi Mubaraka Ng’wada
Mbunge na Waziri wa Sheria na Katiba Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na wananchi kuhusu umuhimu wa mradi wa umwagiliaji
Mhandisi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Ruvuma Lucy Chaula akielezea namna ya mradi wa Umwagiliaji utasaidia kuleta chachu kwa wakazi wa Kata ya Subira na Ruvuma kwa ujumla
Wananchi wakisikiliza maelezo ya umuhimu wa utumiaji wa mradi huo wa maji
Na Regina Ndumbaro – Ruvuma
Wananchi wa Kata ya Subira, Manispaa ya Songea wamepokea kwa furaha hatua ya utiaji saini wa mkataba wa uchimbaji wa visima vya maji ya umwagiliaji, hatua inayotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji katika eneo hilo.
Makabidhiano ya mradi huo yameongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, huku Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Mradi huo ni sehemu ya mpango mpana unaotekelezwa katika mikoa mitatu ya Songwe, Njombe na Ruvuma, ambapo jumla ya shilingi bilioni 518 zimetengwa ili kuhakikisha wakulima wanapata maji ya kutosha kwa shughuli za kilimo.
Hatua hii inatajwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya uhaba wa maji kwa wakulima wadogo na wa kati katika maeneo husika.
Wakizungumza katika hafla hiyo, wananchi wa Kata ya Subira wameeleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo, jambo lililokuwa likikwamisha uzalishaji wao.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, amesisitiza kuwa mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo ya kilimo na uchumi wa wakazi wa Kata ya Subira na maeneo jirani.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji ili kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na tija kwa wakulima.
Kwa upande wake, Oddo Mwisho, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, amewahakikishia wananchi kuwa mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo ana uwezo mkubwa wa kutekeleza kazi kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Amesema kuwa serikali itasimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika ipasavyo na matokeo yanapatikana kama ilivyokusudiwa.
Mkandarasi wa Kampuni ya MNFM Construction Company aliyekabidhiwa mradi huo, ameahidi kuwa kazi ya uchimbaji wa visima itaanza mara moja na itakamilika kwa muda uliopangwa.
Amesema ushirikiano kati ya wananchi na mkandarasi utasaidia kumaliza kazi hiyo kwa ufanisi.
Serikali imesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya maji ya umwagiliaji ni sehemu ya mpango wa kuimarisha sekta ya kilimo na kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula.
Kupitia mradi huu, mikoa ya Songwe, Njombe na Ruvuma inatarajiwa kushuhudia ongezeko la uzalishaji wa mazao, hasa yale yanayohitaji maji mengi kama mboga, matunda na mazao ya biashara.
Wananchi wamehimizwa kushirikiana kikamilifu na mkandarasi pamoja na viongozi wa serikali ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi.
Kwa hatua hii muhimu, Kata ya Subira na maeneo mengine yatanufaika na kilimo cha umwagiliaji, hali itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wake.
Social Plugin