Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MWASSA AKERWA NA WALIMU WASIOTIMIZA WAJIBU WAO

 

*Akemea kisingizio cha walimu kuwa na kazi maalum badala ya kufundisha.

*Awapiga marufuku kupewa ruhusa ya muda mrefu kwenda kufanya kazi maalum.

Na Lydia Lugakila - Bukoba


Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe, Hajjat Fatma Mwassa ametaja kukerwa na baadhi ya walimu wasiotimiza wajibu wao katika kufundisha huku  akisikitishwa na  kiwango cha elimu mkoani humo kuwa cha chini.


RC Mwassa ametoa kauli hiyo katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa(RCC) kikichofanyika Februari 19 katika ukumbi wa Mkoa huo.


Mwassa amesema kuwa katika sekta ya Elimu Mkoa huo haufanyi vizuri hasa kwa shule za msingi na kudai kuwa hali hairidhishi kabisa ambapo ameongeza kuwa katika utafiti alioufanya yeye na timu yake wamebaini wapo walimu hawaendi darasani kufundisha kabisa.


"Kuna Mwalimu tangu shule imefunguliwa mpaka wiki ya mwisho alikuwa ameenda siku mbili tu huku kisingizio kwa Mwalimu au Walimu kikiwa ni KAZI MAALUM.


Mwassa amesema walimu hao wameajiriwa kufundisha hivyo haamini kama kuna kazi maalum ambayo mtu anapewa na asifundishe darasani miezi mitatu nje ya kazi ya Serikali.


Amesema walimu hawapaswi kupewa kazi maalum au ikilazimika kuwepo kazi hiyo maalum basi utaratibu maalum wa kuomba ruhusa ufuatwe kupitia maafisa elimu.


Ameongeza kuwa watumishi wasiotimiza wajibu wao katika utumishi wao hawapaswi kukumbatiwa.


"Bado kuna utoro mwingi lakini tuna namba kubwa ya watoto wanaotoroka shuleni na hawamalizi shule lakini la kusikitisha wanaomaliza hawafanyi vizuri wanafanya vibaya sana."amesema Mwassa.


Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa kwa miaka mitano mfululizo Mkoa wa Kagera umefanya vibaya sana katika Elimu ya msingi.


Amesema kuwa kiwango cha ufaulu badala ya kupanda kinashuka ambapo kwa Mwaka 2024  Mkoa huo umepata ushindi nafasi ya 25 ukiupita Mkoa mmoja.


Mwassa Ameongeza kuwa kama Mkoa huo umetoka nafasi za kushika mkia katika mambo mengine hivyo na katika suala la elimu mapambano ya haraka yanatakiwa kuonekana.


Aidha amewahimiza walimu kutimiza wajibu wao kwa kuwepo darasani kufundisha vipindi vyote alivyopangiwa hadi mtoto ameelewa na matokeo yake ni kufaulu.


Mwassa pia amewataka walimu kujiepusha na udanganyifu wa katika mtihani badala yake wakazanie watoto wasome waelewe ili waweze kufaulu mitihani yao huku akitaka wadau mbali mbali katika kikao hicho kukubaliana ili watoto wa madarasa ya mtihani wabaki/ kuchelewa kutoka shule ili wajifunze ikiwa ni pamoja na kurudi shule siku ya Jumamosi ili wapate masomo ya ziada  wafaulu na kuondoa aibu ya kufeli.


Kwa upande wake mbunge wa Muleba kaskazini Charles Mwijage amekiri kuwepo kwa walimu wasiofika shuleni kwa mwaka mzima ambapo ameshauri kuwa ni vyema maafisa elimu kujenga utamaduni wa kutembelea shule ili kuona na kukagua maendeleo huku akishauri pia kufanyika kwa mabadiliko kwa walimu wakuu wanaokalia vyeo kwa muda mrefu bila shule zao kupata daraja la kwanza hata siku moja.


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Wallace Mashanda amesema kuwa shida kubwa iliyopo katika suala la elimu ni baadhi ya wahusika kutofanya mwendelezo wa kuzingatia mikakati muhimu ya elimu iliyopangwa au inayowekwa huku akiomba mikakati ya ufundishaji izingatiwe na wasiotimiza wajibu wao wachukuliwe hatua za kisheria.


Hata hivyo kupitia kikao hicho cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kupitia Mkuu wa Mkoa wa Kagera kimekubaliana kupiga marufuku Mwalimu kupewa ruhusa ya muda mrefu kwenda kufanya kazi maalum ambapo kazi yake maalum ni kufundisha na si mengineyo.


Wadau hao kwa pamoja wamekubaliana kuandaa mkakati wa kuinua elimu ambapo wadau watashirikishwa na mkakati huo utatekelezwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com