Afisa Habari na Uhusiano Tanesco Mkoani Ruvuma Allan Njiro akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kisiwani C kata ya Subira
Afisa Habari na Uhusiano Tanesco Mkoani Ruvuma Allan Njiro Akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kisiwani C kata ya Subira
Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 blog Ruvuma
Wananchi wa Kata ya Subira katika Mtaa wa Kisiwani C katika Manispaa ya wilaya ya Songea mjini wamepata elimu kuhusu namna ya kuepukana na madhara yanayotokana na uharibifu wa miundombinu ya umeme.
Elimu hiyo imelenga kupunguza ajali zinazoweza kusababisha vifo au majeraha kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na ukataji miti kiholela karibu na nyaya za umeme.
Afisa Habari na Uhusiano Tanesco Mkoani Ruvuma Allan Njiro amewakumbusha wananchi umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme kwa kuwa makini katika shughuli za uzalishaji mali.
Pia amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha watoto wanakaa mbali na maeneo yenye nyaya za umeme ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea.
Katika jitihada za kuongeza usalama wa miundombinu ya umeme, Njiro amesema TANESCO itawasiliana na mafundi maalumu waliopangwa kwa Kata ya Subira ili wananchi waweze kuwatambua.
Ameeleza kuwa iwapo mtu yeyote atabainika akishughulika na transfoma bila kuwa mtaalamu aliyeteuliwa, wananchi wanapaswa kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.
Aidha TANESCO imewahakikishia wananchi kuwa miradi ya REA itaendelea kuimarishwa na ujazilizi wa umeme utafanyika katika maeneo ambayo huduma hiyo ilishafika.
Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa kila kaya inapata umeme wa uhakika kwa maendeleo ya jamii.
Wananchi pia wameelezwa kuwa maombi ya umeme ni bure na yanaweza kufanyika kwa njia mbalimbali ikiwemo simu janja, simu za kawaida, au kwa kutembelea ofisi za TANESCO na tovuti yao rasmi.
Hii ni hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa umeme kwa wananchi wote bila gharama zisizo za lazima.
TANESCO imeahidi kuwa ndani ya mwezi mmoja watafunga nyaya kwenye nguzo katika maeneo husika ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme kwa haraka.
Wananchi wamehimizwa kuwa wavumilivu huku wakisubiri utekelezaji wa mpango huo kufanyika kwa ufanisi.
Kwa wale ambao hawana uwezo wa kufanya wiring kwa nyumba nzima, wameelezwa kuwa wanaweza kuanza na chumba kimoja cha kupokea umeme na baadaye kuendelea kufanya wiring kwa sehemu nyingine kulingana na uwezo wao wa kifedha.
Hii ni fursa kwa kaya nyingi kupata umeme bila kushurutishwa kuwa na gharama kubwa kwa mara moja.
Wananchi wa Kisiwani C wameeleza changamoto zao na pia wametoa shukrani kwa TANESCO kwa kuwapatia elimu muhimu kuhusu utapeli wa umeme.
Wameahidi kushirikiana vyema na TANESCO kwa kila hatua ili kusaidia kuwaibua matapeli wanaojaribu kuwalaghai wananchi kuhusu huduma za umeme.
Diwani wa Kata ya Subira, John Ngonyani, ameishukuru TANESCO kwa kupeleka umeme katika kila mtaa wa kata hiyo, akisema kuwa mitaa yote minane sasa ina umeme.
Amepongeza juhudi za TANESCO kwa kazi nzuri wanayoifanya na pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake katika kuhakikisha umeme unawafikia wananchi wote nchini.
Social Plugin