Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANESCO YATOA ELIMU KWA WANANCHI WA MLETELE KUHUSU UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU YA UMEME



Afisa Habari na Uhusiano Tanesco Mkoani Ruvuma Allan Njiro akizungumza na wananchi wa kata ya Mletele alipokuwa anatoa elimu ya utunzaji wa miundombinu na namna ya kufanya maombi ya kupata umeme
Kaimu afisa Habari huduma kwa wateja Emma Ulendo akizungumza na Wananchi wa kata ya Mletele namna ya kutuma maombi ya kupata umeme
Baadhi ya wananchi wa kata ya Mletele wakisikiliza elimu ya namna ya kufanya maombi ya kupata umeme na utunzaji wa miundombinu ya umeme
Diwani wa kata ya Mletele Mheshimiwa Maurus Nungu akizungumza na wananchi jinsi ya elimu walioipata wananchi waitendee haki


Na Regina Ndumbaro -  Ruvuma. 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limeendelea na kampeni yake ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya umeme. 

Katika ziara yake iliyofanyika kata ya  Mletele, Manispaa ya Songea, TANESCO imewahamasisha wananchi kuhusu njia bora za kupata umeme pamoja na namna ya kulinda miundombinu hiyo kwa maendeleo ya jamii.

Afisa Habari na Uhusiano wa TANESCO mkoani Ruvuma, Allan Njiro, amewaeleza wananchi wa Mletele jinsi wanavyoweza kutuma maombi ya kupata umeme. 

Amefafanua kuwa ili kupata huduma hiyo, mwombaji anapaswa kufanya maombi rasmi, kuhakikisha nyumba yake imefanyiwa wiring kwa viwango vinavyotakiwa, na kulipa gharama zinazohitajika kwa matumizi ya nyumbani, gharama ni shilingi 321,000, huku kwa viwanda ikiwa shilingi 912,000. 

Amebainisha kuwa kwa sasa, muda wa kuunganishiwa umeme umepunguzwa hadi siku nne hadi saba baada ya kukamilisha malipo.

Aidha, Njiro amesisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu ya umeme kwa kuzuia wizi wa mafuta ya transfoma na nyaya, pamoja na ukataji miti kiholela karibu na maeneo ya miundombinu hiyo. 

Amewaomba wananchi kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa wanapogundua watu wasiofahamika wakijihusisha na vitendo vya uharibifu au wizi wa miundombinu ya umeme.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Habari wa Huduma kwa Wateja TANESCO, Emma Ulendo, ametoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya wiring kwa kutumia wakandarasi waliosajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). 

Amesisitiza kuwa maombi ya umeme yanaweza kufanywa kwa kufika ofisi za TANESCO mkoani Ruvuma au kupitia simu za mkononi kwa kutumia mfumo wa NIKONEKTI, ambao unawarahisishia wananchi kujaza fomu za maombi kwa njia ya kidigitali.

Ulendo pia amewahimiza wananchi kulipa gharama za umeme kwa njia za kielektroniki ili kuepuka matapeli. 

Amesema kuwa baada ya kufanya malipo, wateja wanapaswa kusubiri kwa muda mfupi kabla ya kuunganishiwa huduma. 

Aidha, amehimiza wale ambao bado hawajafanya maombi ya umeme kufanikisha hatua hiyo, akieleza kuwa uwepo wa umeme huongeza thamani ya ardhi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Wananchi wa Mletele waliopata elimu hiyo wameishukuru TANESCO kwa kuwapatia maarifa sahihi kuhusu huduma za umeme na namna ya kulinda miundombinu hiyo. 

Wamesema kuwa wataendelea kushirikiana na mamlaka ili kuhakikisha miundombinu ya umeme inabaki salama na inawanufaisha wote.

Diwani wa Kata ya Mletele, Mheshimiwa Maurus Nungu, amewapongeza TANESCO kwa juhudi zao za kutoa elimu kwa wananchi. 

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora ya umeme.

Diwani huyo ameeleza kuwa mradi wa umeme katika kijiji cha Mletele umegharimu shilingi milioni 144,712,000 hadi kukamilika kwake. 

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha huduma za umeme zinafika kwa wananchi wote ili kuboresha maisha yao na kukuza uchumi wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com