WIKI YA AZAKI 2024 KUANZA RASMI SEPTEMBA 9-13 JIJINI ARUSHA


Na: Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM 

Washiriki zaidi ya 500 kutoka Asasi za Kiraia (AZAKI), Sekta Binafsi, Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo wanatarajiwa kushiriki maadhimisho ya Wiki ya AZAKI 2024, itakayofanyika kuanzia Septemba 9 hadi 13 Jijini Arusha. 

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Agosti 23, 2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa The Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge, amesema kuwa, wiki hiyo imebebwa na kauli mbiu ya Sauti, Dira na Thamani, ikiendana na wakati uliopo na matukio yanayoendelea nchini, ambayo ni pamoja na uchaguzi wa Serikali za mtaa utakaofanyika mwaka huu, uchaguzi mkuu wa mwakani na Dira ya Taifa ya Maendeleo.

 “Tupo kwenye kipindi muhimu sana kwenye demokrasia yetu kama nchi, kwa sababu mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mtaa, wote mnafahamu, pia mwakani tuna uchaguzi mkuu, lakini la jambo la kipekee sana, mwakani tunatarajia kuzindua dira ya maendeleo ya Taifa ya 2050 ambayo ni fursa adimu sana inayokuja mara moja kwa muda mrefu. Fursa hii kutokana na umuhimu wake si budi sauti za wananchi zikasika kuchangia maoni yao wenye, kwani dira ya Taifa inapaswa itokane na sauti, mawazo, mitazamo na maoni ya wananchi”, amesema Rutenge. 

Aidha, Rutenge ameongeza kuwa, wiki hiyo pia itakuwa na mijadala mbalimbali inayohusu shughuli za AZAKi nchini, maendeleo ya jamii na ushirikiano baina ya Asasi za Kiraia, Serikali na sekta binafsi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika kusaidia na kuwezesha watu wenye ulemavu wa macho nchini (CBM), Nesia Mahenge, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya wiki ya AZAKi 2024, amesema kuwa kuelekea katika wiki hiyo maandalizi yamekamilika, ambapo amewashukuru wadau wote waliojitokeza kudhamini na kuwezesha maadhimisho hayo.


Aidha, Mahenge ameeleza kuwa, katika wiki hiyo itayaleta pamoja makundi mbalimbali ikiwemo vijana, jamii, makundi maalum na wadau mbalimbali watakaojadiliana kwa pamoja mada zinazohusiana na kaulimbiu ya maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya wiki ya AZAKI 2024 ni ya sita kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post