TARURA YAPONGEZA UJENZI BARABARA YA MWAJIJI SHINYANGA






Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

Wananchi wa Kijiji cha Mwajiji kilichopo Kata ya Lyabusalu, Wilaya ya Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga wametoa pongezi kwa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kwa ujenzi wa barabara ya Mwajiji yenye urefu wa KM 5.
Pongezi hizo zimetolewa kijijini hapo, ambapo wananchi walieleza changamoto walizokuwa wakizipata kabla ya ujenzi wa barabara hiyo, ikiwemo wanawake kujifungulia njiani kutokana na barabara hiyo kuwa na tope wakati wa masika.

“Wakati wa masika tulikuwa tunapata shida sana kupita kwenye barabara hii, kutokana na barabara kujaa tope, hivyo vyombo vya usafiri kushindwa kupita, na wakati mwingine vilikuwa vikitumia muda mrefu kutoka eneo moja kwenda eneo lingine,” amesema Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwajiji, Maligisa Mbuya.
Ameendelea kusema kuwa, baadhi ya wakina mama walijifungulia njiani kutokana na adha ya barabara hiyo, ambapo walikuwa wakitumia muda mrefu njiani, na kucheleweshwa kufika katika kituo cha afya.

“Kwa sasa barabara inapitika vizuri, na imefika mpaka kituo cha afya, hivyo tatizo la wakina mama kujifungulia njiani halitakuwepo tena, tunaishukuru serikali kwa kutukumbuka wananchi wa Mwajiji,” amesema mwenyekiti huyo.

Aidha, amesema kuwa, barabara hiyo itafungua uchumi wa kijiji hicho, kwani wakazi wengi wa eneo hilo ni wakulima, hivyo uwepo wa barabara utawarahisishia usafirishaji wa mazao yao kutoka mashambani mpaka kwenye masoko.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Avith Theodory amesema katika mkoa wa Shinyanga TARURA ina hudumia mtandao wa barabara wenye Km. 5,220, ambazo kati ya hizo Km. 40.9 ni barabara za lami, Km. zaidi ya 2,000 ni barabara za changarawe na Km. zaidi ya 3,100 ni barabara za udongo.

Mhandisi Theodory amempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia TARURA fedha ili kuweza kutekeleza majukumu yake.

“Miaka mitatu nyuma, TARURA ilikuwa na bajeti ya takribani bilioni 7.2, lakini kwa kipindi hiki cha miaka mitatu, bajeti imeongezeka mpaka kufikia bilioni 18, ambazo zimefanya maendeleo makubwa ya miundombinu ya barabara katika mkoa wa Shinyanga,” amesema Mhandisi Theodory.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post