NAIBU WAZIRI WA NISHATI AWAHAKIKISHIA UPATIKANAJI WA HUDUMA YA UMEME HALMASHAURI YA MSALALA

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Naibu Waziri wa Nishati nchini Mheshimiwa Judith Kapinga amewahakikishia wananchi upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye maeneo yote ya vijiji na vitongoji vilivyopo halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ifikapo 2025.

Ameyasema hayo Julai 02, 2024 wakati wa ziara yake ya ukaguzi ndani ya halmashauri ya Msalala ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ndani ya wilaya ya Kahama.

Mheshimiwa Kapinga amesema dhamira ya serikali ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kufikiwa na huduma ya umeme ifikapo 2025 kama inavyosema ilani ya chama hicho na kuwaahidi wananchi kuwa ataendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme ili kufanikisha dhamira ya serikali na kuwaondolea changamoto wananchi.

“Tumekuja hapa kuhakikisha changamoto za wakazi wa Msalala zinapatiwa ufumbuzi , mengi yamezungumzwa ikiwemo mafanikio na changamoto, ni kweli yapo maeneo yenye uhitaji mkubwa wa umeme hususani maeneo yenye kukua kwa kasi, kama serikali tunaendelea kusambaza huduma ya umeme na kutoa kipaumbele kwenye maeneo yenye uhitaji na niwatoe hofu nitahakikisha sehemu zote ambazo zimetajwa kuwa na changamoto ya umeme hadi ifikapo 2025 maeneo yote yatakuwa yamefikiwa na umeme”, amesema Mhe. Kapinga.

Awali akieleza hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye halmashauri hiyo mbunge wa jimbo la Msalala Mheshimiwa Iddi Kassim amesema kulingana na kukuwa kwa kasi kwa halmashauri hiyo kwenye maeneo mbalimbali inasababisha uhitaji mkubwa.

“Tunaishukuru serikali yetu kwa kutuletea umeme vijijini lakini bado kuna changamoto ya uhitaji, kati ya kata 18 za halmashauri hii zipo kata ambazo zinakuwa kwa kasi sana ikiwemo Kagongwa ambapo bado mtandao wa umeme ni mdogo ukilinganisha na uhitaji uliopo hivyo tunaiomba serikali yetu kupitia Naibu Waziri wa Nishati dada yangu Mheshimiwa Judith Kapinga tuongezee angalau ili wananchi hawa waweze kufanya kazi zao kwa uhuru bila kuhofia lolote",

 "Lakini pia mimi kama Mbunge na mwakilishi wa wananchi nitaendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha fedha anazoleta katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinafanya kazi kama ilivyokusudiwa na serikali”, ameongeza Mheshimiwa Iddi.

Akizungumza kwa niaba ya serikali ya mkoa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Wakili Julius Mtatiro ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo usambazaji wa umeme maeneo ya vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini REA na kuipongeza REA kwa kuendelea kusambaza umeme kwenye maeneo mbalimbali kupitia wakandarasi waliowaweka. 

Naibu Waziri wa Nishati Nchini Mheshimiwa Judith Kapinga akizungumza wakati wa ziara yake ndani ya Halmashauri ya Msalala.Mbunge wa jimbo la Msalala Mheshimiwa Iddi Kassim akizungumza wakati wa ziara hiyo ndani ya halmashauri ya Msalala.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza wakati wa ziara hiyo ndani ya halmashauri ya Msalala.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kahama Mhe. Thomas Muyonga akizungumza wakati wa ziara hiyo.


Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Dr. Christina Mnzava akizungumza na wananchi wa halmashauri ya Msalala.


Meneja wa shirika la umeme Tanzania  TANESCO wilayani Kahama Tumaini Chonya akizungumza.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post