HAKUNA MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA TANZANIA BILA TTCL

 


Na Mwandishi Wetu Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), leo Mei 16, 2024 ametembelea Banda la Maonesho la Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL wakati Shirika hilo liliposhiriki maonesho ya Taasisi, Kampuni na Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Katika maonesho hayo TTCL kupitia Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Peter Ulanga amepata fursa ya kumwelezea Mhe. Waziri Mkuu miradi ya kimkakati inayoendeshwa na Shirika hilo ikiwa ni pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo mahiri cha kutunza kumbukumbu (NIDC)


Kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano TTCL imeziunganisha nchi 8 za ukanda wa Afrika Mashariki huku zaidi ya Wilaya 92 zikiwa zimeunganishwa na Mkongo huo na hivyo kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, Afya na kijamii kufanyika kidigitali.



Awali , Waziri wa Habari,Mawasiliano na teknolojia ya Habari,Nape Nnauye ,akiwasilisha Bungeni Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Wizara hiyo amesema TTCL imefanikiwa kukusanya shilingi 135,216,317,693 hadi kufikia Aprili 2024 katika mwaka wa fedha 2023/24 sawa na asilimia 56.34 ya lengo lililopangwa la kukusanya Shilingi 240,000,000,000 kutokana na huduma za mawasiliano, ukodishaji wa vifaa vya mawasiliano, upangishaji majengo na ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Pia Waziri Nape ameongeza kuwa hadi kufikia Aprili 2024 shirika hilo lilifanikiwa kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Wilaya 22 za Karatu, Mbulu, Longido, Hai, Mwanga, Pangani, Muheza, Lushoto, Kibiti, Mtama, Nachingwea, Newala, Mbinga, Ludewa, Ileje, Vwawa, Mbogwe, Msalala,Tarime, Sengerema, Rorya na Ngara.

"TTCL imefanikiwa kuunganisha watumiaji 12,584 wa huduma za faiba mlangoni sawa na asilimia 63 ya lengo ,"

Na kuongeza kuwa "Shirika limefanikiwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya Wi-Fi katika maeneo manne ya umma ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo
cha Uhasibu Arusha (IAA), Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Uwanja wa Benjamin
Mkapa Jijini Dar es Salaam,"amesema Nape.


Aidha Waziri Nape amesema kuwa TTCL ilifanikiwa kufanya tafiti mbili za kuridhika kwa wateja ambapo lilisajili wateja 102,850 wapya wa T-PESA kwa ajili ya kutumia huduma za kifedha za T-PESA na Kuunganisha Taasisi sita za Serikali na Binafsi kwa ajili ya huduma za malipo ya mkupuo (bulk disbursement).

Vilevile ameeleza kuwa shirika hilo lilifanikisha kusainiwa kwa Mikataba ya mauzo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi za Uganda wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 28.8, Malawi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.5 na Kampuni ya Airtel wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4.8.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo Bi. Zuhura Muro ,amesema kuwa hakuna mapinduzi ya kiteknolojia Tanzania bila TTCL hivyo kwa bajeti ya Wizara hiyo itawezesha kujenge ustahimilivu wa mawasiliano kwani watahakikisha huduma za mawasiliano za uhakika zinawafikia wananchi.

" Kwanza bajeti hii ina maana kubwa sana kwetu kama shirika kwa sababu Bunge linaelewa adhma ya Rais Samia ya kutaka kuhakikisha changamoto zote za mawasiliano zinatatuliwa katika nchi yetu na kazi hiyo inafanywa na sisi TTCL,"amesema Bi.Zuhura


Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa watanzania baada ya kuona Bajeti yao imepita kwa kishindo waamini kuwa TTCL inakwenda kuboresha miundombinu ya mawasiliano ili kufikia katika uchumi wa Kidigiti.

"Sisi tunausika na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano hivyo watanzania ambao wameshughudia bajeti hii inapita kwa kishindo naomba wajue kwamba sisi tutajenga miundo mbinu ambayo itawawezesha wao kufikia malengo katika ukuzaji wa uchumi wa Kidigitali," ameeleza Mhandisi Ulanga


Maonesho hayo yaliandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuzishirikisha Taasisi, Mashirika na Kampuni zilizochini ya Wizara hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post