TMA YATOA TAARIFA KUHUSU MWENENDO WA KIMBUNGA HIDAYA


Dar es Salaam, 02 Mei 2024 Usiku: 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu. Kimbunga “HIDAYA” kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufika saa tatu usiku wa tarehe 02 Mei 2024 kilikuwa umbali wa takriban Kilomita 402 Mashariki mwa pwani ya Mtwara. 

 Nguvu ya kimbunga HIDAYA imeendelea  kuimarika na kuwa kubwa zaidi, ambapo hadi kufikia usiku huu kasi ya upepo katika kimbunga  imeimarika na kufika Kilomita 110 kwa saa na inatarajiwa kuendelea kuimarika zaidi katika kipindi cha saa 24 zijazo. 


Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga “HIDAYA” kuendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania na kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 mwezi Mei 2024. Hata hivyo, kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.

 

Uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu na pwani ya nchi yetu unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani. 


Vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara. Ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 Mei 2024. 


USHAURI: Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post