THTU YASHAURI MAMBO 10 KUHUSU BIMA YA AFYA 


Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dkt. Paul Loisulie,akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Uchambuzi na Mapendekezo ya hoja za NHIF na Pensheni nchini Tanzania.

Na Alex Sonna - DODOMA

CHAMA Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) kimeshauri mambo kumi kuhusu bima ya afya kwa wote huku ikiitaka Serikali iwe na hasira na wivu juu ya rasilimali zinazotapanywa kila mara katika mifuko hiyo na kuchukua hatua ya kukomesha.

Ushauri huo umetolewa leo Aprili 24,2024 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa THTU Taifa,Dkt.Paul Loisulie,alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari.

Dk Loisulie amesema Serikali imepitisha sheria ya Bima ya Afya kwa wote ya mwaka 2023 kwa lengo la kuweka masharti ya kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kupitia bima ya afya.

Pia kuanzisha mfumo wa bima ya afya kwa wote, kuweka masharti ya kupanua wigo wa huduma mbalimbali za afya na kuweka masharti mengineyo yanayohusiana na hayo.

Amesema bima ya afya kwa wote maana yake ni utaratibu ulioidhinishwa kwa mujibu wa Sheria unaowezesha kila mwananchi kupata huduma za afya kupitia bima hiyo bila kikwazo cha fedha pindi anapozihitaji huduma hizo.

Mwenyekiti huyo amesema pamoja na changamoto zote na dalili isiyo nzuri juu ya Bima ya Afya kwa wote, THTU wanaamini kuna mambo ya kufanyika kwa utashi sahihi na nia thabiti ili kuwezesha Bima ya Afya kwa wote ifanye kazi kwa ufanisi mkubwa.

Amesema Serikali iwe na hasira na wivu juu ya rasilimali zinazotapanywa kila mara katika mifuko hiyo na kuchukua hatua ya kukomesha.

Pia ni wakati muafaka kama nchi tukiongozwa na viongozi wetu kufanya maamuzi ya makusudi kabisa kutumia sehemu ya mapato ya vyanzo vingi vya rasilimali vilivyopo kugharamia huduma za afya.

"Tuelekeze macho na nguvu zetu zote kwa rasilimali kama madini, bandari, misitu, utalii na nyingine. Tuache kabisa kukodolea macho vyanzo vile vile vinavyoongeza mzigo hasa kwa wafanyakazi na wanajamii,"amesema

Pia THTU imeshauri Serikali iwe na hasira na wivu juu ya rasilimali zinazotapanywa kila mara katika mifuko na kuchukua hatua ya kukomesha isisubiri ripoti ya CAG bali ichukue hatua mapema.

Serikali pia iepuke utaratibu wake wa kukopa au kujichotea pesa kutoka kwenye mfuko ili pesa hizo zitumike kugharamia huduma za afya na si vinginevyo.

Vilevile Bunge litimize wajibu wake kikamilifu katika kutunga sheria rafiki kwa wafanyakazi na wanajamii pamoja na kuisimamia serikali katika usimamizi wa mifuko husika.

"Bunge halipaswi kuwa sehemu ya kulalamika bali kutatua changamoto zinazojitokeza,"amesema

Pia upo ulazima wa Wafanyakazi, wanajamii na wanufaika wote wa Bima kuamka usingizini na kuacha tabia ya kugugumia chini kwa chini huku Mfuko ukiteketea.

"Ijengeke tabia ya kuhoji na kushinikiza uwajibikaji pale matumizi mabaya na usimamizi usioridhisha inapobainika na mamlaka zinazoaminika kama CAG"amesema

Vilevile fanyike mijadala ya wazi na shirikishi kuhusu uhai wa mfuko mara kwa mara ili kubaini changamoto na namna ya kuzitatua badala ya kuachia mfuko peke yake.

Amesema hiyo itahusisha pia kutumia ripoti za kitaalamu za tathmini juu ya mwenendo wa mfuko.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post