NEMC YATOA ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA ZEBAKI KWA WACHIMBAJI WADOGO


BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limetoa elimu ya matumizi salama ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo na wasambazaji wa mgodi wa Mwakitolyo uliopo Kata ya Mwakitolyo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ili kupunguza madhara ya zebaki kiafya na kimazingira.

Aidha, NEMC kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wanatekeleza mradi wa kudhibiti matumizi ya Zebaki (EHPMP) unaotekelezwa kwa Mikoa  ya Geita, Mbeya, Singida, Mwanza, Mara, Songwe na Shinyanga kwa Ufadhili wa Benki ya Dunia.

Akiendesha mafunzo hayo leo Afisa Ufuatiliaji na Tathimini wa mradi huo kutoka NEMC, Hassan Maalim amesema, lengo kuu la utekelezaji wake ni kuwa na mazingira yenye viwango vinavyokubalika vya zebaki kwa mujibu wa mkataba wa Minamata kuhakikisha matumizi ya Zebaki yanadhibitiwa.

Amesema, wachimbaji wengi wanafanya kazi zao katika mazingira magumu na hatarishi bila kuchukua tahadhari yoyote wakati wa kuchakata dhahabu, na wengi hawavai gloves mikononi kwa kuhofia dhahabu kubaki bila kujua wanahatarisha usalama wa maisha yao, na kuwakumbusha kuchukua tahadhari.

Nae Meneja wa Ukaguzi na Usajili kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali Bi. Magdalena Mtenga amebainisha baadhi ya madhara yanayowapata wachimbaji pale wasipochukua tahadhari kuwa ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu, figo kuathirika na kuchanganyikiwa.

Madhara mengine ni kupoteza kumbukumbu, kupata msongo wa mawazo muda wote, kupoteza uwezo wa macho kuona vema, mikono kutetemeka, kupunguza nguvu za kiume, kuharibika kwa mimba na watoto kuzaliwa na utindio wa ubongo.

Mtenga amewataka kujenga tabia ya kufanya vipimo mara kwa mara ili kujua viwango vya zebaki mwilini mwao na pale vitakapozidi wafuate ushauri wa madaktari watakaopewa.

Mmoja wa wachimbaji walioshiriki mafuzo hayo Juma Daudi amesema kuwa hakuwa anajua madhara ya zebaki kama yanaweza kusababisha mimba kuharibika na kupoteza uwezo wa kuona kwani amekuja kuthibitisha hilo baada ya kumuona mmoja wao ameathirika na zebaki na kuwa na rangi mbili mwilini mwake na kuahidi kuchukua tahadhari muda wote awapo kazini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post