REA KUWEZESHA UPATIKANAJI NISHATI SAFI VIJIJINI

 

Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Wakala wa Nishati vijijini(REA) kupitia mpango wake wa kuwezesha upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia vijijini imejipanga kuendelea kutoa hamasa na elimu ya matumizi ya tekonojia rahisi na nafuu kwa Watanzania kuweza kutumia nishati safi ya kupikia ili kuendeleza uhifadhi mazingira na kutunza afya za watanzania.

Hayo yameelezwa Jijini hapa na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu, Mhandisi Advera Mwijage kwenye Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia na kueleza kuwa wamejipanga kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo ili watanzania wa hali zote waweze kumudu gharama yake.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa,amesema REA imekuwa mstari wa mbele kuwasaidia Waendelezaji wa teknolojia za nishati safi pamoja na Miradi inayolenga  kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia.

"REA inatekeleza jukumu la kuhakikisha nishati za aina zote zinapatikana vijijini na kwa Watu wote,tumekuwa mstari wa mbele kuwasaidia Waendelezaji wa teknolojia za nishati safi pamoja na Miradi inayolenga kwenye kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia lengo ni kuona watanzania wanaachana na nishati zinazoharibu mazingira na kuingia kwenye ulimwengu wa nishati safi,"amesisitiza 

Licha ya hayo ameeleza kuwa, "REA kwa kushirikiana na STAMICO imefadhili ununuzi wa mashine kubwa tatu kwa ajili ya kuzalisha makaa ya mawe,Mradi huo, umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 5 na sisi kama Wakala tuna hamasisha matumizi ya mkaa mbadala ambao ni salama kama chanzo cha nishati safi ya kupikia”ameeleza Mhandisi huyo. 

Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Wakala huo umetoa zaidi ya mitungi ya gesi ya kupikia 158,100 kwa Wananchi wa vijijini kama sehemu ya hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuongeza kuwa mitungi zaidi ya laki 4 itatolewa kupitia utaratibu huo. 

Amesema mbali na ugawaji wa mitungi ya gesi, REA imeanza kutekeleza program ya kusambaza gesi asili kwa Wananchi wa vijijini wa mkoa wa Pwani na Lindi, Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 6.8 ambapo kwa kuanzia kaya zaidi 980 zitaunganishwa kwenye mtandao wa gesi asilia kwenye nyumba zao.

"Mradi mwengine ni wa kuwaunganisha Wananchi wa vijijini katika mkoa wa Pwani na Mtwara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),Mradi huu una thamani ya shilingi bilioni 13.5 ambapo kwa kuanzia kaya zaidi ya 1,400 zitanufaika, amefafanua.

Amesema REA pia inatekeleza Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, ambapo Tanzania kuna magereza zaidi ya 129 ambapo imeelezwa kuwa matumizi ya kuni pekee yake ni zaidi ya asilimi 93. Mradi huo umeanza kutekelezwa na utagharimu shilingi bilioni 40.

"Miradi mwingine unaofanana na huo ni ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo kambi 26 zitanufaika na Mradi huo uliotengewa zaidi ya bilioni 3.5 ambapo utaanza kutekelezwa hivi karibu, " amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments