KIMBISA AZINDUA BARAZA LA WAZEE KATA YA IPAGALA, AWATWISHA MZIGO WA MAMBO MATATU KUONGEZA USTAWI WA CCM

 

Na Dotto Kwilasa, DODOMA.. 

Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi(CCM)Mkoa wa Dodoma Adam Kimbisa amezindua Baraza la Wazee Kata ya Ipaga huku akiwatwisha mzigo wa mambo matatu ikiwemo uingizaji wanachama wapya, kuhamasisha watu kujiandikisha kupiga kura na  kuhamasisha watu kujitokeza kupiga kura wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa. 

Akizindua Baraza hilo leo Machi 16,2024 katika Shule ya mfano ya Mtemi Mazengo iliyopo Kata ya Ipagala, Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa iwapo mambo hayo matatu yatafanikiwa yatasaidia kuongeza ustawi wa chama hicho na kuleta ari ya wananchi kuwajibika kupiga kura. 

Pamoja na mambo mengine ametoa Wito kwa watanzania waliotimiza vigezo vya kupiga kura , kujiandikisha ili kupata haki ya kupiga kura  kuwachagua viongozi bora watakaowezesha maendeleo kwa taifa. 

Ameeleza kuwa idadi ya wanachama wa Chama hicho kwenye Kata hiyo ni 7000 na kueleza kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wananchi waliopo kwenye Kata hiyo ambayo ni wananchi 50000 na kutoa rai kwa viongozi wa Kata kuhamasisha zaidi watu kujiunga na Chama hicho. 

Kimbisa pia amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hasan kuwa hana mpinzani kwenye kinyang'anyiro cha nafasi ya Urais na kwamba 
huyo ndiye mwenye sifa ya kuwaongoza watanzania . 


Akizungumzia kuhusu Baraza hilo Kimbisa amesema,ni muhimu wazee kuenziwa kwa kuwa  ndio waliochangia kuleta uhuru kwa kuchangia pesa zao kufanikisha harakati za uhuru huku akiwataja kuwa wao ndio wanaojua maana ya uhuru na amani iliyopo ikiwa ni pamoja na kutunza Siri na mali za nchi kwa ustawi wa jamii. 

Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kuwaomba Viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kuwashauri waamini wa dini zao kushiriki kwenye uchaguzi na kuwa na maamuzi ya kuwachagua viongozi wenye maono na Tanzania. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ipagala kwa tiketi ya Chama cha mapinduzi Gombo Kamuli Dotto amesema uundaji wa Baraza hilo ni tiba  kwani unaenda kuimarisha umoja wa wananchama wa CCM na kukiimarisha Chama. 

Ametumia nafasi hiyo pia kueleza fursa ambazo Serikali imekuwa ikiwapatia wananchi wa Kata hiyo  kuwa zimewagusa moja kwa moja sambamba na kutatua kero ambazo zilikuwa zikikwamisha maendeleo yao.

Amesema kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Serikali ya awamu ya Sita kukamilika kwa wakati na kuwaletea maendeleo wananchi wa Kata hiyo, Chama cha mapinduzi kina uhakika wa kupata kura za kishindo kwenye eneo hilo. 

Ameeleza kuwa Kata hiyo yenye mitaa 8,kwa uchaguzi wa mwaka 2020 iliongoza kwa kura nyingi na kwamba imejiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa na kuhakikisha chama hicho kinakuwa kinara. 

Kuhusu miradi ya Maendeleo kwenye Kata hiyo,Diwani huyo ameeleza kuwa Serikali imeahidi kumaliza changamoto zote kwa kusogeza huduma kwa jamii na kuongeza fursa kwa wajasiriamali, kuongeza ufaulu wa wanafunzi, kujenga kituo cha afya huku kukiwa na mpango wa kujenga kituo cha polisi. 

Amesema kuwa mafanikio hayo yanampa nafasi ya yeye kusimama kifua mbele kuwaomba wananchi kukichagua chama cha mapinduzi ambacho Serikali iliyo chini yake imejitahidi kutatua matatizo na changamoto kwa wananchi kwa asilimia 90.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa changamoto zote kwenye Kata hiyo ikiweno masuala ya upimaji wa ardhi zinaendelea kutatuliwa huku akitumia kuiomba  Serikali kuongeza watumishi kukamilisha upimaji wa haki kuondokana na udanganyifu unaopoteza stahiki za wananchi. 

Amesema kwa Matokeo ya mwaka 2023,ufaulu kwa wanafunzi uliongezeka na kutolea mfano Shule ya msingi Ilazo ambayo ilifaulisha darasa zima na kwamba kila matokeo yanapotoka  huwa anatoa motisha kwa walimu jambo linasaidia kuchochea ufaulu. 

Pamoja na hayo ameeleza kuwa Kata hiyo imejipambanua kwa kufuata maelekezo mbalimbali yanaoyotilewa na Serikali kuhusu uhifadhi wa mazingira ambapo imeshiriki kampeni ya kupanda miti elfu 17 kupitia kuwezesha usafi wa mazingira. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la wazee Kata ya Ipagala Yusuf Semgunda
amewatoa hofu wazee hao kuwa uzee ni hazina na kwamba huanzia miaka 60 na kuendelea. 

Amesema yeye binafsi anajivunia kuwa mzee baada ya kumaliza kulitumikia taifa kwa miaka mingi na kufichua siri ya yeye kuendelea kuwa na furaha imetokana na kufuta taratibu za kiafya zinavyoelekeza. 

Pamoja na mambo mengine Baraza hilo la wazee linatajwa kuwa litawasaidia kubadilishana mawazo na kupeana taarifa na kuwaunganisha ikiwa ni pamoja na kukishauri chama  juu ya mambo mbalimbali kwa kujenga mtizamo sahihi kwa jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post