KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA SERIKALI UWEKEZAJI SEKTA YA AFYA

 


Na Mwandishi wetu- GEITA

Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus  Nyongo amewataka wanafunzi kuzingatia masomo yao ili kutimiza ndoto zao pamoja na kuchukua tahadhari ili kuepuka kupata  maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

Mwenyekiti alitoa kauli hiyo wakati Kamati  ilipotembelea  na kukagua shughuli za mwitikio wa UKIMWI zinazotekelezwa na wadau kwa uratibu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Halmashauri ya Wilaya ya Geita Vijijini  Mkoani Geita ambapo ilifanya ziara Kata ya Bugulula,  Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Bugulula kuona namna ambavyo wanafunzi hao wamejifunza jinsi ya kupambana na kudhibiti ugonjwa hatari wa UKIMWI.

Aliwataka wanafunzi hao kutokuwa waoga kutoa taarifa kwa walimu au wazazi wao pale wanapoona kuna watu wanawasumbua ikiwa ni pamoja kuwashauri wazazi wao kuwahimiza kutumia dawa  kwa wanafunzi ambao wamepata maambukizi na kuepuka unyanyapaa kwa wagonjwa wenye maambukizi ya VVU.

“Tumetembelea maeneo mbalimbali kujionea uwekezaji mkubwa unaofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya afya na leo tupo Geita Kata ya Bugulula, Mhe Rais anatutaka watanzania wote tuwe na afya bora ndio maana amewekeza kwenye vituo vya afya, Zahanati, Hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali za Rufaa,” Alisema Mhe. Nyongo.

Pia alipongeza uanzishwaji wa mradi wa Timiza Malengo unaotekelezwa katika Halmashauri hiyo  kwa lengo la kuwasaidia wasichana balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 walioko shuleni na walio nje ya mfumo wa elimu kuwezeshwa kijamii na kiuchumi  kwa kuwapatia mitaji ya kiasi cha shilingi 250,000 kila mmoja kwa wasichana  571 ili kujikimu kimaisha wakiwa salama dhidi VVU na UKIMWI.

Akiwasilisha Taarifa kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mkuu wa shule ya Msingi Bugulula, Bw. Peter Miayo alisema Mafunzo ya timiza malengo yalitolewa kwa walimu  katika shule hiyo kwa lengo la kutoa elimu kwa walimu wengine pamoja  wanafunzi ambao tayari wamefikia katika kipindi cha balehe kwa jinsia zote (wavulana na wasichana) ambao ndio walengwa wa mradi huo.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mkoa wa Geita Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Saidi Mkumba, katika sekta ya UKIMWI alieleza kwamba  hali ya maambukizi ya VVU katika Mkoa wa Geita Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI wa mwaka 2022/23 unaonesha kuwa kiwango cha maambukizi katika Mkoa huo ni asilimia 4.9 kwa watu wa umri wa miaka 15-49 ukilinganishwa na kiwango cha maambukizi kitaifa ambayo ni asilimia 4.4.

“Mkoa wa Geita unakadiriwa kuwa na takribani watu 90,282 wanaishi na VVU hadi kufikia Disemba 2023, ambapo jumla ya WAVIU 85,945 ambao ni sawa na asilimia 95.2 ya WAVIU wote wanatambua hali zao kati ya hao WAVIU 80,945 sawa na asilimia 94.1 wako kwenye huduma za tiba na matunzo ya ARV, asilimia 97.4 ya walioko kwenye tiba wamefikia kiwango cha ufubavu wa VVU,” Alifafanua Bw. Mkumba.

Vile vile Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameupongeza Mkoa huo kwa kuendelea kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga ambapo kwa mwaka 2022 jumla ya kina mama wajawazito 106,162 walijifungua huku mwaka 2023 kina mama wajawazito walijifungua 116,990.

“Vifo vya watoto wachanga mwaka 2022 walikuwa na vifo 905 mwaka 2023 vifo 814 kwahiyo hongereni sana  watendaji na viongozi wote wa sekta ya afya. Changamoto iliyopo ni kwenye lishe asilimia 38.6 ukilinganisha na kiwango cha Taifa ambacho ni asilimia 30,”Alieleza.

Aidha  Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga aliwahimiza wanafunzi hao kuendelea kuweka bidii katika masomo yao na kutowanyanyapaa waathirika wa maambukizi ya VVU pamoja na kuwasihi wanufaika wa Mradi wa Timiza Malengo ambao ni wasichana balehe kutoa elimu kwa wenzao.

Wakiongea mbele ya Mwenyekiti wa Kamati na Wajumbe Walengwa ( Wasichana Balehe na Wanawake Vijana) hao wameishukuru Serikali kwa kuja na wazo hilo ambalo limewakomboa na kuepusha na tabia hatarishi ambazo zingeweza kuwasababishia kupata maambukizi ya VVU.

Ikumbukwe Mradi wa Timiza Malengo ulianza kutekelezwa na serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita 2022/2023 pamoja na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali ya AMREF Tanzania pamoja na TAYOA, Ukiratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS)  kwa ufadhili wa mfuko wa Dunia (Global Fund) ambao lengo lake ni kuwasaidia wasiachana balehe, na wanawake vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 walioko shuleni kuhitimu elimu na walio nje ya mfumo wa elimu kuwezeshwa kijamii na kiuchumi ili kujikimu kimaisha wakiwa salama dhidi ya VVU na UKIMWI.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post