GBT YASAJILI KAMPUNI 91 ZA MICHEZO YA KUBAHATISHAMkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), James Mbaga, Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha maofisa wa Bodi hiyo, waandishi na wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam leo Machi 6,2024.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodaus Balile, akizungumza kwa niaba ya Wahariri walioudhuria Kikao hicho muda mfupi kabla ya kuhitimishwa kwa kikao kazi hicho Jijini Dar es Salaam.

Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabatho Kosuri, akizungumza alipokuwa akiongoza mijadala, ikiwemo maoni na maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiulizwa na Wahariri, pamoja na Waandishi wa Habari katika kikao hicho.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF, Anitha Mendoza, (kulia), pamoja na baadhi ya Wahariri wa Habari katika Mkutano huo.

(PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM

Mkurugenzi Mkuu wa BODI ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, (GBT), James Mbaga, amesema kuwa hadi kufikia Juni 2023, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), imesajili jumla ya kampuni 91 zinazoendesha biashara za aina mbalimbali ya michezo ya kubahatisha nchini.

Mbaga amebainisha hayo alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu mafanikio na utendaji wa Taasisi hiyo, katika kikao kazi kati ya Bodi hiyo, Wahariri wa vyombo vya habari, kilichofanyika leo Machi 6,2024 Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa mwendeshaji sharti awe na leseni hai iliyotolewa na Bodi hiyo, na kwamba michezo hiyo hairuhusiwi kuendeshwa katika maeneo yaliyopo Karibu na nyumba za ibada, shule, usalama, yasiyofikika kirahisi na maeneo ya kuendeshea biashara ya michezo ya kubahatisha, na kwamba kwa maeneo yaliyoruhusiwa sharti yawe yamesajiliwa na Bodi hiyo.

"Watoto wenye umri chini ya miaka 18 hawarusiwi kushiriki michezo ya kubahatisha kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

"Mwendeshaji sharti awe na leseni hai iliyotolewa na Bodi, hivyo michezo hii hairuhusiwi kuendeshwa katika maeneo ambayo yamekatazwa kisheria" amesisitiza Mbaga.

Ameongeza kuwa, katika Jiji la Dar es Salaam zipo kasino nane, wakati Arusha na Mwanza kila mkoa zikiwa na kasino moja.

"Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na kasino nane, wakati Mwanza na Arusha kila mkoa una casino moja, sawa na asilimia 90 ya kasino zipo Dar es Salaam," amesema Mbaga.

Amefafanua kuwa, kuna aina mbalimbali ya michezo ya kubahatisha ambayo ni michezo ya kibiashara kama kasino inayochezwa kwenye majumba maalum na mtandaoni, slot inayochezwa zaidi kwenye maduka maalum na baa, ubashiri wa matokeo ya michezo mtandaoni na madukani na bahati nasibu ya jumbe fupi za simu (sms lotteries).

Ameongeza kuwa, mchango wa sekta katika mapato ya serikali kodi imeongezeka kutoka shilingi bilioni 33.6 mwaka 2016/17 hadi kufikia shilingi bilioni 170.4 kwa mwaka 2022/23, ambapo ni sawa na ongezeko la wastani wa asilini 407.1 kwa mwaka katika kipindi hicho.

"Sekta ya michezo ya kubahatisha Tanzania tumefanikiwa kuzalisha ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi zaidi ya 25,000. Hivyo sekta hii imefanikiwa kutoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa ajira nchini," amesema Mkurugenzi mkuu huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post