KULWA LENIS JISHANGA MWENYEKITI MPYA WA CHAMA CHA USHIRIKA SHINYANGA 'SHIRECU'


Ndg. Kulwa Lenis Jishanga, Mwenyekiti Mpya Bodi ya SHIRECU (1984) LTD ataongoza kwa muda wa miaka mitatu

Na Paul Kasembo - SHINYANGA RS.

MKUTANO Mkuu wa 29 wa Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga [SHIRECU (1984) LTD] umemchagua Ndugu Kulwa Lenis Jishanga kuwa Mwenyekiti wake mpya baada ya uchaguzi uliowahusisha wajumbe wa SHIRECU tarehe 26 Machi, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika jengo la SHIRECU hapa Manispaa ya Shinyanga, huku Ndugu Jishanga akiwataka wanaSHIRECU kuwa wamoja na waitumikie Ushirika kwa moyo mmoja, uzalendo na kujituma ili waweze kuirejeshea hadhi yake ya zamani.

Uchaguzi huu uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa zamani Ndg. Josephati Limbe, umejumuisha wajumbe wote huku Limbe akisema kuwa huu ni utekelezaji wa kawaida wa matakwa ya Ushirika ili kuweza kutekeleza mipango na mikakati iliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambayo ni pamoja na ununuzi wa Kiwanda kipya cha kuchambua Pamba, ununuzi wa Pamba Mbegu, ujenzi wa Ghala la kisasa katika Kanda ya Solwa na Ukumbi wa kisasa wa Mikutano utaokuwa na uwezo wa kuchukua watu elfu 5.

"Ndugu wajumbe, pamoja na mamno mengine, lakini pia Ushirika unaleta kwenu mipango mkakati kadhaa ili muweze kuridhia itekelezwe ikiwemo ununi wa Kiwanda kipya cha kuchambua Pamba na unnuzi wa Pamba Mbegu kwa msimu wa mwaka 2024/2025, na hii i akwenda sambamba na ombi la Bodi kwenu ili mridhie ukopaji wa fedha zaidi ya Bil. 5 kutoka Benki ya TADB ili kuweza kutekeleza miradi hii ya kimkakati," amesema Limbe.

Awali Mhe. Julius Mtatiro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha alisema kuwa, wanaushirika wamepata bahati sasa kwakuwa wamepata DC ambaye ni mwanaushirika pia, hivyo atahakikisha kuwa Vyama vya Ushirika na wakulima wanakuwa na tija katika pamoja na kuirejesha SHIRECU katika hadhi yake kama zamani.

Aidha Kaimu Meneja SHIRECU Bi. Asnath Changamike alisoma taarifa huku akiwaomba wajumbe kuridhia mapendekezo ya makisio ya bajeti kwa mwaka 2024/2025 yenye zaidi ya Bil. 1.4 ambapo wajumbe walipitisha pia bajeti hii.

Mkutano umewapatia dhamana Ndg. Kulwa Jishanga kuwa Mwenyekiti, Bi. Naomi Masega - Makamu Mwenyekiti, na wajumbe ni Mussa Robert, Dasse Dotto, Fransic Daniel na Philipo Lunegula.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments