WATENDAJI KATA NA MAAFISA KILIMO WA HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA WATAKIWA KUSIMAMIA UKUSANYAJI WA MAPATO

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Bw. Kisena Mabuba amewataka Watendaji wa Kata na Maafisa Kilimo kusimamia ukusanyaji wa mapato na kudhibiti upotevu wa fedha katika maeneo yao ya kazi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato. 

Agizo hilo limetolewa Februari 19, 2024 wakati wa kikao kazi  kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.

“Kwenye suala la mapato, hatuna aibu, hali ya  mapato katika  halmashauri yetu ndugu zangu ni mbaya, mtu yeyote anayekiuka utaratibu wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali mkamateni na waelimisheni wananchi wajibu wajibu wao wa kutoa ushuru.....haiwezekana halmashauri yetu kutofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato.” Alisisitiza

Mabuba amesema haridhishwi na hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri hiyo na anachukizwa na kitendo cha mashine za kukusanya mapato kutofanya kazi vizuri. Hivyo,  ameelekeza ukaguzi wa mashine hizo ili kubaini ambazo hazifanyi kazi vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuchukua hatua stahiki. Vile vile, ameelekeza ununuzi wa mashine mpya za kukusanya mapato ufanyike ili kuendana na mahitaji halisi.

Akiainisha vyanzo vya mapato katika halmshauri hiyo, Bw. Mabuba amesema kuwa halmashauri hiyo pamoja na vyanzo vingine inategemea mapato ya mazao na mifugo. Kila Afisa Kilimo, Afisa Mifugo na Mtendaji Kata asimame kwa nafasi yake na kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali hayapotei na kusisitiza kuwa makusanyo yote yawekwe benki kwa wakati bila kucheleweshwa.

Aidha, Mabuba amemwelekeza Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo  na Uvuvi  Bw. Edward Maduhu kuhakikisha halmashauri inapata taarifa ya mavuno yanayoanza kuvunwa ili kuweka msisitizo wa ukusanyaji mapato katika maeneo hayo.

Awali akielezea vipaumbele vya halmashauri wakati wa uwasilishaji wa rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa mwaka 2024/2025, Bw. Mabuba alimweleza Mkuu wa Mkoa Shinyanga kuwa halmashauri  hiyo imejipanga kwa kuweka mikakati madhubuti ambayo itasaidia  kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Baadhi ya mikakati aliyoiainisha ni pamoja na kufuatilia na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza ili kuziba mianya ya wizi,  kutoa elimu kwa wafanyabiashara, kuandaa kanzi data ya wafanyabiashara wote, kuwezesha wakusanya mapato kwa kuwapatia vitendea kazi muhimu na kuongeza mashine za kukusanya mapato ( POS) .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post