MAJAJI WAANZA KUCHAMBUA KAZI KUTAFTA WAANDISHI MAHIRI HABARI ZA TAKWIMU ZINAZOHUSU WANAWAKE NA UONGOZI ZANZIBAR

JOPO la majaji ambao ni wataalamu na wajuzi katika fani ya habari wameanza kazi ya kuchambua kwa kina kazi za Waandishi wa Habari wanaowania Tuzo ya Umahiri katika uandishi wa habari za takwimu zinazohusu masuala ya Wanawake na Uongozi Zanzibar.

Majaji hao wanatoka katika vyombo mbalimbali vya habari, ikiwa ni pamoja na magazeti, redio, televisheni, na mitandao ya kijamii.

Uteuzi huu umefanyika kwa kuzingatia sifa za usiri na uadilifu ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa ufanisi.

Majaji hao watafanya kazi kwa siku tano (5) ya kupitia kazi na kuandika ripoti kamili inayoonesha mchakato pamoja na washindi wa kwanza hadi watatu kwa kila eneo.

Vigezo vinavyoangaliwa ni pamoja na makala hizo kuzingatia mada husika lakini pia kuwepo kwa ubunifu wa mada, habari iliyokuwa na vyanzo tofauti vya habari pamoja na makala au vipindi hivyo kuzingatia masuala ya jinsia na makundi ya pembezoni.

Tuzo hizo ambazo kauli mbiu yake ni “kalamu yangu, mchango wangu kwa wanawake”, zinalenga kuhamasisha waandishi wa habari kutumia kalamu na vyombo vya habari kuelimisha umma umuhimu wa nafasi za wanawake katika uongozi, hivyo kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali za ngazi za maamuzi.

Kalamu za waandishi wa habari hazina budi kulenga katika kuinua wanawake ili waweze kushiriki katika uongozi ikiwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha usawa na haki kwa wanawake na wanaume kama inavyoeleza katika katiba ya Zanzibar ya 1984.

Hata hivyo TAMWA, ZNZ inawashukuru Waandishi wa Habari Zanzibar kwa kuonesha mwitikio wa kuandika habari za takwimu kuhusu wanawake na uongozi, ambapo kumekua na ongezeko la kazi mwaka huu ambazo ni 529 ukilinganisha na mwaka jana ambapo waandaaji walipokea kazi 421.

Aidha TAMWA ZNZ inatoa wito kwa Waandishi wa Habari kuendelea kutumia kalamu zao kuandika makala na kuandaa vipindi kuhusu takwimu za wanawake na uongozi, huku wakisisisitiza umuhimu wa kuinua wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Tuzo hizi zinatolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL). Mradi huo unatekelezwa na TAMWA Zanzibar, Jumuia ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), pamoja na Jumuia inayojihusisha na Mazingira, Usawa wa Kijinsia, na Utetezi Pemba (PEGAO), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Nchini Tanzania.

Imetolewa na kitengo cha habari,

TAMWA ZNZ.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post