BYABATO : MAREHEMU BALOZI DKT. KAMALA AMELITUMIKIA TAIFA KWA NGUVU ZOTE, TUTAMKUMBUKA KWA MENGI


Na Mariam Kagenda _ Kagera

Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini ambaye pia ni Naibu waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Adv Stephen Byabato amewahimiza wananchi wa wilaya ya Missenyi kuendelea kumuombea Marehemu Balozi Dkt. Diodorus Kamala aliyetangulia mbele ya haki na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha aliyoishi hapa Duniani.


Mhe.Byabato amesema hayo wakati akitoa salamu za pole za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Balozi Diodorus Kamala ambapo amesema kuwa ameleta salamu za pole kutoka kwa Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuondokewa na kiongozi mahiri na shupavu aliyewahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali kwa nyakati tofauti tofauti kwenye serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


Ameongeza kuwa pia ameleta salamu za pole kutoka kwa wasaidizi wa Mheshimiwa Rais akiwemo Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango , Waziri mkuu Kassim Majaliwa,Naibu waziri mkuu Dkt Dotto Biteko pamoja na Waziri wa wizara ya mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba ambaye alitamani kuwepo lakini hakuweza kujumuika nao kutokana na majukumu aliyoagizwa ambapo viongozi hao wote wamemtuma afikishe salamu za pole kwa mke wa Marehemu, watoto,Ndugu na wanaKagera wote kwa ujumla .


Mhe. Byabato amesema kuwa Balozi Dkt Kamala alikuwa mwanafamilia katika wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo alitumia kipaji chake kutumikia Taifa la Tanzania kwa nguvu zake zote na uzalendo mkubwa kwa kusimamia masilahi ya Taifa na pale alipokabidhiwa jukumu la Kitaifa alilifanya kwa moyo wote kwa kutumia elimu yake na karama yake ya uongozi kushauri katika masuala mbalimbali.


Marehemu Balozi Dkt Diodorus Kamala aliteuliwa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Naibu waziri wa ushirikiano wa Afrika mashariki mwaka 2005 mpaka 2008 na baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki kuanzia mwaka 2008 mpaka mwaka 2010.Aidha amesema kuwa watamkumbuka kwa mengi ikiwa ni pamoja na jinsi alivyosimamia kidete msimamo wa Tanzania kuwa suala la Ardhi ya Tanzania au nchi nyingine lisiingizwe katika itifaki ya soko la pamoja pia kusimama na kuhakikisha ujenzi wa Jengo la makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unaanza, linajengwa na kukamilika kwa viwango vinavyostahili ambapo mpaka sasa linatumika


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments