Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo juzi. Waliokaa ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (kushoto) na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji, Solomon Shati.
Maofisa kutoka halmashauri hiyo wakifuatilia matukio
Wawakilishi wa Barrick katika kikao hicho wakifuatilia mijadala ya madiwani
***
Katika kudhihirisha kuwa Uwekezaji katika sekta ya madini unazidi kunufaisha wananchi, mgodi wa Barrick North Mara uliopo Tarime mkoani Mara mwaka huu utatoa kiasi cha shilingi bilioni 9 za uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi katika halmashauri ya wilaya ya Tarime.
Fedha hizo ziliidhinishwa na kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Nyamwaga na kuhudhuriwa na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara na viongozi wengine wa Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Kiles, alieleza kikao cha baraza hilo kuwa asilimia 60 ya fedha hizo za CSR kutoka Barrick North Mara, imeelekezwa kwenye vijiji 77 na asilimia 40 itapelekwa kwenye vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi huo.
“Kati ya asilimia 60 iliyoelekezwa kwenye vijiji 77, asilimia 30 imeelekezwa kwenye miradi ya kimkakati ya halmashauri na 30 imeenda kwenye vijiji husika,” amefafanua Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga.
Kiles pia alitoa wito kwa madiwani kuwatangazia wananchi miradi hii inayotekelezwa na fedha za uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka mgodi wa North Mara ili wafahamu umuhimu wa kuwepo mgodi huu katika eneo lao “Hakikisheni mnafanya mikutano ya hadhara ya wananchi kwenye kata zenu kwa ajili ya kuongelea miradi ya CSR ili wananchi waelewe faida ya kuwa na mgodi huu” alisisitiza.
Akizungumzia ufanisi wa miradi inayotekelezwa na fedha za CSR, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Vijijini, Solomon Shati, alisema ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya CSR katika wilaya hiyo umekuwa ukizidi kuwa bora mwaka hadi mwaka na kwa sehemu kubwa utajikita kwenye miradi ya kijamii ambayo ni vipaumbele vya wananchi wa maeneo husika, kama vilivyowasilishwa na wawakilishi wao [madiwani].
“Tunatekeleza mpango shirikishi, hatufanyi kama halmashauri - bila kupata mawazo ya wananchi na ninyi madiwani ambao ndio wawakilishi wao, na maelekezo ni kwamba mipango yote ijikite katika kutatua kero za wananchi na vipaumbele vyao,” alisema Shati.
Alisema Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na mgodi imezidi kuboresha utekelezaji wa miradi ya CSR, “ukichukua miradi ya mwaka 2019/2020 wakati CSR inaanza, ukailinganisha na miradi ya CSR kipindi hiki ni vitu viwili tofauti, na tumeendelea kushirikiana na wenzetu wa mgodi wa North Mara vizuri,” alisema Shati.
Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, alitoa ombi kwa madiwani hao kutangaza kwa wananchi miradi ya CSR katika kata zao, pamoja na kusaidia kukemea vitendo vya uvamizi mgodini vinavyofanywa na makundi ya watu wanaojulikana kama 'intruders'.
“Kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye jamii, na mnafahamu hata sasa kuna miradi ya bilioni 7.3 ambayo tunaikamilisha,” alisema Uhadi.
Uhadi alisema bado uvamizi wa mgodi ni tatizo na aliwaomba madiwani kuwaelimisha wananchi madhara ya vitendo hivi ambavyo vinaondoa utulivu katika uzalishaji na kusababisha hasara ikiwemo kuhatarisha maisha ya watu.
“Pia, tunawaomba mkatangaze kwenye kata zenu kwamba miradi hiyo inayotekelezwa chini ya CSR imetokana na fedha zilizotolewa na mgodi, maana kuna wananchi hawana taarifa kuwa mgodi unatoa fedha kwa jamii kwa ajili ya kuwaletea maendeleo sambamba na kuboresha maisha yao”, alisema Uhadi.
Mgodi huo ambao upo Nyamongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, na unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.