MBUNGE MTATURU ATAJA MAMBO MANNE YALIYOMO KWENYE MISWADA YA SHERIA ZA UCHAGUZI

 

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,akichangia Miswada ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023,Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023 bungeni jijini Dodoma.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameeleza mambo manne yaliyopendekezwa kwenye miswada mitatu ya Sheria zinazodhamira kuleta mageuzi kwenye uchaguzi na kisiasa ikiwemo uwepo wa kamati ya usaili inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023,Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

Akichangia miswada hiyo Januari 30,2024,bungeni Jijini Dodoma,Mtaturu amesema eneo la Tume Huru ya Uchaguzi lilikuwa linapigiwa kelele na wadau wengi na Rais Samia Suluhu Hassan ameliona hilo na kuridhia mabadiliko hayo.

“Ni Marais wachache wenye nguvu ambao wanaweza kukubali baadhi ya mambo yake yafanywe na watu wengine,Mhe.Rais wetu amekubali kwamba kuwe na Kamati ya Usaili ambayo itamsaidia kuwachuja watu,kamati ambayo imebeba watu waaminifu wa level ya juu kabisa ambao wataenda kufanya kazi hiyo kwa niaba ya Mh Rais."

“Kamati hii ya Usaili ambayo imetajwa tusipoiamini tutamuamini nani, maana yake ni kwamba tutakapokuwa tumekubali Sheria hii tutakuwa tumekubali Kamati hii ya Usaili itakayomsaidia sana Mh Rais kuondoa maneno ambayo yamekuwepo kwamba amekuwa akiteua peke yake,jambo ambalo sio kweli kwak uwa Rais ni taasisi lakini sasa amekubali,hivyo Kamati itateua au kupendekeza majina matatu na yatapelekwa kwa Rais,”amesema.

Jambo la pili alilochangia ni kuhusu sifa za viongozi wa Kamati ya Usaili ambao kupitia Sheria hiyo wanatakiwa kuwa majaji na kusisitiza kuwa Sheria hiyo ikipitishwa watakuwa na Tume Bora ya Uchaguzi ambayo itaenda kuwa na jibu la manung’uniko yaliyoliyokuwepo siku za nyuma.

Mtaturu ametaja jambo la tatu ni kuhusu wagombea kupita bila ya kupingwa ambapo mwanzoni kulikuwa na kelele lakini kupitia sheria hiyo kelele hizo zimesikilizwa.

“Viongozi wengi wameeleza kuwa haiwezekani kukawa na mgombea mmoja akapita bila ya kupingwa hivyo kupitia hii sheria akitokea mgombea mmoja lazima apigiwe kura ya ndio ama hapana ili kuamua ama kubariki kuwa huyu sasa amechaguliwa kwa kupiga kura,”amesema.

Amesema hatua hiyo itaondoa hofu ile iliyokuwepo mwanzoni kwamba watu wanapitishwa tu ili waende wakawe viongozi bila ya kuwa na ruhusa kutoka kwa wananchi.

Jambo la nne ni kuhusu Usawa wa Kijinsia ambalo limezingatiwa katika Sheria ili kuondoa manyanyaso yaliyokuwepo katika baadhi ya meneo.

“Baadhi ya wanawake wazuri katika maeneo fulani fulani lakini wameshindwa kuchaguliwa kwa sababu tu ni wanawake,lakini kumekuwa na mfumo dume katika maeneo ya jamii yetu ambayo hayaamini katika mwanamke kuwa kiongozi kwa hiyo kupitia Sheria hii itavilazimisha vyama vya siasa kuweka wagombea ambao ni wanawake au kama walivyosema wengine hata wanaume ambao hawakubaliki,”.amesema Mtaturu.

Amewaomba watanzania kuiunga mkono serikali na kuipitisha miswada hiyo ambayo itaimarisha demokrasia nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post