PROFESA TIBAIJUKA ATOA ZAWADI KWA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI NA UFADHILI WA MASOMO KWA WANAFUNZI WA KIKE, MTIHANI KIDATO CHA PILI



Profesa Anna Tibaijuka akitoa Motisha kwa wanafunzi waliofanya vizuri na walimu wao wa masomo

Na Mariam Kagenda - Muleba

Profesa Anna Tibaijuka  aliyewahi  kuwa Waziri wa Ardhi na Mbunge Mstaafu wa  Jimbo la Muleba Kusini  ametoa motisha kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mtihani wa kidato cha pili mwaka 2023 pamoja  na walimu wao wa masomo Katika shule ya Sekondari Anna Tibaijuka baada ya shule hiyo kufanya vizuri kwenye matokeo yao.

Wakati akitoa motisha hiyo Profesa Tibaijuka amewataka wanafunzi wa shule hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mitihani yao na kusoma kwa bidii kwani elimu ndio msingi wa maisha yao.

 Licha ya kutoa motisha hiyo ya shilingi milioni 1 kwa wanafunzi waliofanya vizuri pamoja na kila mwalimu wa somo pia ametoa ufadhiri wa masomo kwa wanafunzi wakike waliopata daraja la kwanza katika mtihani wa kidato cha pili kwenda kusoma katika shule za bweni za Kajumulo iliyoko Bukoba na Barblo Johansson iliyoko jijini Dar es Salaaam.


Ameongeza kuwa licha ya kustaafu siasa lakini hajastaafu kuwajibika katika jamii na ni mdau mkubwa wa elimu hasa kwa watoto wa kike hivyo ataendelea kutoa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika shule hiyo na kutoa ufadhiri wa masomo kwa wanafunzi wa kike wanaofanya vizuri katika masomo yao.

Amesema kuwa hasa kilichomsukuma kutoa zawadi hizo ni kuwapa nguvu walimu na kuleta hamasa kwa wanafunzi kusoma kwa bidiii na kuwaimiza wazazi kuwajibika kwa upande wao kwani nao ni walimu hasa watoto hao wanapokuwa nyumbani na kutowaachia walimu pekee jukumu la malezi.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya Sekondari Anna Tibaijuka ambayo ni shule ya Serikali bi. Kagemulo Lupanka amemshukuru Profesa Tibaijuka na kusema kuwa watahakikisha shule hiyo inaendelea kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.

Aidha wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha pili kwa mwaka 2023 katika shule hiyo ni 202 na wote wamefaulu kujiunga na kidato cha tatu mwaka 2024 ambapo wanafunzi 14 wamefaulu kwa daraja la 1, 20 daraja la 11,61 daraja la 111 na 107 daraja la IV.
Profesa Tibaijuka akitoa Motisha kwa mkuu wa shule ya Anna Tibaijuka
Profesa Anna Tibaijuka akiwa na walimu wa shule ya Sekondari Tibaijuka

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post