WAZIRI KAIRUKI AENDELEA KUHAMASISHA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UTALII



Na Happiness Shayo- Arusha 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki ameendelea kuweka wazi fursa mbalimbali zilizoko kwenye Sekta ya Utalii na kuhamasisha wawekezaji wa Kitaifa na Kimataifa kuwekeza katika Sekta hiyo ili kuongeza mapato yatokanayo na Utalii nchini.

Ameyasema hayo usiku wa Desemba 1,2023 kwenye ukumbi wa Gran Melia jijini Arusha, katika hafla ya Epic Tanzania Tour Gala Dinner iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau.

 “Kutokana na utajiri wa rasilimali, vivutio vya utalii wa wanyamapori, fukwe , utamaduni na nyinginezo nyingi, kuwekeza nchini Tanzania kunaleta faida kubwa hasa chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,”  Kairuki amesisitiza.

Ametaja baadhi ya  fursa za uwekezaji katika Sekta ya Utalii ikiwa ni pamoja na huduma za malazi, shughuli za utalii, usafirishaji, vituo vya mikutano,  migahawa ya kimataifa, utalii wa pwani, hoteli zenye hadhi ya juu, shughuli za baharini, na huduma za ufukweni kwa wasafiri wa baharini Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, amesema ili kurahisisha watalii kutembelea vivutio vilivyoko nchini Tanzania, Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini akitolea mfano ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayolenga kuunganisha Jiji la Dar es Salaam ambalo ni lango kuu la watalii kwenda njia ya kati na kusini, Shirika la Ndege nchinj., kupanua uendeshaji wa safari za ndege, kuboresha Kituo cha 3 cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, na kukarabati viwanja vingine vya ndege vya kikanda vinalenga kuboresha utalii na vituo vingine vya biashara nchini Tanzania.

Katika hatua nyingine, Kairuki amesema kupitia programu ya filamu ya "Tanzania Royal Tour", iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali, idadi. watalii wameongezeka maradufu . 

Ametumia fursa hiyo kuzishukuru kampuni za Insider Expeditions kutoka Amerika ambayo imefanya kazi kwa kushirikiana na Gosheni Safaris kutoka Tanzania katika kufanikisha tukio hilo.

“ Tunatambua na kuthamini juhudi zenu na tunawaomba wadau wengine kuungana nasi katika kukuza na kuendeleza sekta ya utalii kwa kutangaza bidhaa mbalimbali za utalii na tunaahidi  kujitolea kufanya kazi kwa karibu na washirika wengine wote” Mhe. Kairuki amesema.

Waziri Kairuki pia amepongeza ujio wa wadau zaidi ya 80 na Gwiji wa Tennis, John McEnroe ambao watashiriki katika mashindano ya tenisi yatakayofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Naye, Gwiji wa Tennis John McEnroe ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri na maandalizi mazuri kwa ajili ya mashindano ya tenisi yatakayofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Ninafurahishwa na hili suala la kuutangaza Utalii pamoja na mchezo wa Tennis nchini Tanzania ” amesema McEnroe.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post