ZIMBABWE YAPONGEZA MIFUMO YA UTUNZAJI TAARIFA ZA MADINI TANZANIA


Na. Wizara ya Madini , Dodoma.

Ujumbe wa Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Maendeleo ya Migodi nchini Zimbabwe umeipongeza Wizara ya Madini kuwa na mfumo mzuri wa Usimamizi wa Leseni za Madini ujulikanao _Mining Cadastre Information Management System_ (MCIMS) unaotumia Teknolojia shirikishi katika utunzaji wa taarifa za madini.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 5 , 2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Uendeshaji Migodi Wizara ya Madini nchini Zimbabwe Charles Simbalache wakati mafunzo kuhusu mfumo wa MCIMS unaotumika Tanzania.


Ikiwa siku ya kwanza ya mafunzo maalum kwa ujumbe huo, Wataalam wa Wizara ya Madini Tanzania wakiongozwa na Kamishna Msaidizi Francis Mihayo wameeleza juu ya mfumo mzima wa MCIMS unavyofanyakazi kuanzia hatua ya awali za kujisajili huku akieleza faida zinazopatikana ndani ya mfumo huo.


Sambamba na hapo, ujumbe huo umejifunza kuhusu Sheria za Madini na Kanuni zake, Muongozo wa Sera ya Madini, mifumo ya utoaji leseni pamoja na aina zake .


Pia, ujumbe huo umeelezwa jinsi Wizara ya Madini inavyosimamia maendeleo ya migodi nchini na namna ya kujikinga na majanga katika migodi na jinsi inavyosimamia utunzaji wa mazingira maeneo yenye migodi.


Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Teknolojia ya Mawasiliano Wizara ya Madini Zimbabwe, Bi. Susane Kachote, amesema kuwa lengo la ziara hii ni kupata mafunzo kuhusu namna bora kuimarisha na kuweka teknolojia ya kuweza kusimamia mnyororo mzima wa sekta.


"Pamoja na usimamizi pia tukiwa na mifumo mizuri itasaidia kuzuia mianya ya utoroshaji madini nchini Zimbabwe" Kachote amesema


Awali, akifungua mafunzo hayo Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Madini Francis Mihayo amesema kuwa Tanzania inatajwa kufanya vizuri katika sekta ya madini kutokana na kuwepo kwa mifumo mizuri ya usimamizi kuanzia ngazi ya uchimbaji mdogo mpaka mkubwa, jambo linalopelekea mataifa mengine kuja Tanzania kujifunza namna ya usimamizi wa mifumo hiyo.


Kutokana na kufanana kwa jiolojia nchi ya Tanzania na Zimbabwe zimekuwa zikishirikiana katika kubadilishana uzoefu katika sekta ya madini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post