WIZARA YA KILIMO YAJA NA MIKAKATI YA KUONGEZA UTOSHELEVU WA CHAKULA NCHINI

 

Mkurugenzi wa Idara ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Ndg.Nyasebwa Chimagu,akizungumza katika Mkutano wa Mafunzo kwa wadau wa kilimo yaliyoandaliwa na AMDT, Novemba 22,2023 jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.

Na Okuly Julius, Dodoma


WIZARA ya Kilimo imeweka mikakati ya kuongeza hali ya utoshelevu wa chakula kutoka asilimia 124 iliyopo sasa hadi kufikia asilimia 130 kama ilivyoeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Akizungumza katika Mkutano wa Mafunzo kwa wadau wa kilimo yaliyoandaliwa na AMDT, Novemba 22,2023 jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, Mkurugenzi wa Idara ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Ndg.Nyasebwa Chimagu amesema kuwa Muelekeo wa kilimo nchini ni KILIMO BIASHARA hivyo chochote kinachozalishwa kiwe ndio chakula, ajira na biashara.

 

‘’Baada ya kujihakikishia kuwa utoshelevu wa chakula nchini ni wa kuridhisha sasa Wizara ya Kilimo imeweka mikakati ya kuhakikisha kilimo kinakuwa cha tija na inawanufaisha wananchi wapate kipato,ajira na wapunguze umasikini ndio maana tunashirikiana na wadau kama AMDT kuhakikisha wakulima wetu wanapata mafunzo ya namna ya kuzalisha kwa tija na kupata masoko kwa ajili ya mazao yao,’’

 

Na kuongeza kuwa “lengo letu kama sekta ya kilimo ni kuhakikisha wakulima wetu wanazalisha chakula cha kutosha na kuilisha dunia na hiyo ndio ahadi yetu kuilisha dunia na kwa mikakati iliyopo na jinsi hali ya upatikanaji wa chakula ilivyo kwa sasa naamini tutafanikiwa kuilisha dunia kibiashara”amesema Nyasebwa

 

Nyasebwa amesema kwa sasa Wizara ya kilimo inaandaa MASTER PLAN ya maegeuzi ya kilimo nchini  ambayo itakuwa inaitwa  ( TANZANIA AGRICULTURE MASTER PLAN 2050) ambayo itajumuisha malengo yaliyopo katika AGENDA 10/30 na mpango wa pili wa maendeleo  unaondelea.

 

Amesema kuwa wakati serikali ikielekea kuhitimisha Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2020 – 2025 ndio mwanzo wa maandalizi wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa  mpaka 2050 hivyo nayo Sekta ya Kilimo inaandaa mpango wao ambao utasomana na mpango wa nchi katika sekta zote.

 


“tumekuwa tukiandaa mikakati karibia kila mwaka ila haitekelezwi hivyo malengo ya Sekta ya kilimo ni kuona sasa inaanza kutekeleza mikakati yote na kuhakikisha changamoto zilizopo katika sekta hii zinatatuliwa,”

 

Na kuongeza kuwa “niwaombe wadau wa sekta ya kilimo ikiweo AMDT kuchangia maoni na mapendekezo katika MASTER PLANI YA KILIMO ili kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa na wakulima wakanufaike na kilimo na wajiajiri wapate kipato na kupunguza umasikini,”ameeleza Nyasebwa

 

Amesema moja ya changamoto inayokwamisha upatikanaji wa masoko ya uhakika nje ya nchi ni kukosekana kwa tija hii inasababishwa na kutokidhi viwango vinavyotakiwa kuanzia kweye ubora,wingi,mabadiliko ya bei sokoni na kuhakikisha kuwa muda wote tunasambaza bidhaa masokoni.

 

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa AMDT Dk.Mary Shetto alisema wanashukuru ushirikiano wanaopata kutoka wizara kilimo katika miradi wanayotekeleza katika maeneo mbalimbali.

 

Alisema  ushirikiano huo umesaidia AMDT kufikia wadau wengi na kwa usahihi zaidi.

 

“AMDT imeendelea kushirikiana na wizara katika kupanga mikakati wa nazao mbalimbali tunaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana ili kuhakikisha tunafikia lengo tulilojiwekea,”alisema

 

Awali akizungumza katika Mafunzo hayo kwa wadau wa kilimo, Mratibu wa Mradi wa kujenga kesho Bora (BBT)  Ray Mark amezungumzia utaratiu wa vijana wanaotekeleza mradi huo kupelekwa kwenye mafunzo maalum ya Ukakamavu na Uzalendokweny Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)  Ili wasiyatelekeze mashamba watakayopewa bali wyathamini na kuyatunza.

 

Mark ametoa kauli hiyo baada ya mdau wa kilimo kutoka Taasisi ya Farm Afrika, Meshack Panga  kuhoji ulazima wa vijana hao kupelekwa JKT na kuwaacha wakulima wengine wakifanya shughuli za kilimo bila mafunzo ya uzalendo.

 

Panga amesema kama ni suala la uzalendo kila mkulima apelekwe JKT ili kujifunza uzalendo na siyo vijana wanaotekeleza mradi wa BBT peke yake.

 

"Kama ni suala la uzalendo mbona wakulima wengine hawapelekwi JKT, basi na wao wapelekwe ili kujifunza huo uzalendo," amesema Panga.

 

Akijibu hoja hiyo Mark amesema vijana hao wanapelekwa JKT kwa sababu mashamba hayo hawajayagharamikia bali wamepewa bure tofauti na wakulima wengine ambao wanamiliki mashamba kwa nguvu zao.

 

Amesema vijana hao hawana uchungu na mashamba hayokwa sababu hawajatumia nguvu zozote kutapata hivyo wakiachwanbila kupewa mafunzo ya uzalendo wanaweza kuyatelekeza tofauti na wakulima wengine.

 

"Hata ukiangalia watu wenye vitu vya urithi huwa hawana uchungu navyo wanaweza kurithishwa lakini mwisho wa siku wasivithamini wakaviuza kwa sababu hawajui thamani yake," amesema Mark.

 

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya kuwafanya vijana hao waone mashamba hayo ni mali yao na si ya mtu mwingine hivyo wan wajibu wa kuyatunza na kuyalima maisha yao yote.

 

Mratibu huyo amesema vijana hao watapewa vyumba kwenye maeneo ya mradi ili waweze kuyasimamia mashamba yao lengo ni kuhakikisha hakuna shamba linalotelekezwa kwa sababu zozote zile.

 

Amesema baada ya vijana hao kumaliza mafunzo ya ukakamavu na uzalendo kutoka JKT ndipo watakapokabidhiwa mashamba hayo kwa ajili ya kuendeleza kilimo ambapo baadhi ya wadau wameshajitikeza na kupendekeza aina za mazao kwa ajili ya malighafi za viwanda vyao.

 

Naye Meneja wa mikopo kutoka benki ya CRDB Kanda ya kati, Sarah Mabula amewataka vijana hao kujiunga kwenye vikundi ili waweze kukopesheka na kuongeza mitaji kwenye uzalishaji wa mazao watakayolima kwa sababu benki hiyo inakopesha wakulima walioko kwenye vikundi peke yake.

 

Amesema wakulima wanaokopesheka ni wale ambao mashamba yao yanatambuliwa kisheria kwani wakulima wengi mashamba yao hayajarasimishwa bali wanamiliki kimila hivyo wakijiunga kwenye vikundi inakuwa rahisi kwao kutambulika na kukopesheka.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post