GRUMETI FUND YAWAFUNDA WANAFUNZI WA KIKE NA KIUME SERENGETI

 

 


KAMPUNI ya Grumeti Fund  kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii katika kuhakikisha inamkomboa mtoto wa kike kifikra imewakusanya pamoja wanafunzi wa kike  zaidi ya 390 na wavulana 435 Kwa wakati tofauti kutoka shule za sekondari Ikoma, Manchira, Robanda na Sedeko zilizopo wilayani Serengeti kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazomkabili mtoto wa kike pamoja na utatuzi wa changamoto hizo.

Katika makongamano hayo yaliyofanyika
katika shule za Sekondari Ikoma na Robanda ziliopo Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya jamii kutoka Grumeti Fund Bi. Frida Mollel amewataka wasichana  kujitambua na kujua thamani yao sambamba na kutumia elimu wanayoipata ili iweze kuleta tija na mabadiliko chanya katika jamii.

"mnathamani kubwa katika nchi hii, na mtambue kuwa mnaweza kuwa mtu yeyote kwenye dunia hii kama mkipenda, ukitaka kuwa yeyote ipo katika mikono yako mkijitambua" alisema Bi. Frida Mollel.

Katika kongamano hilo Kampuni ya Grumeti Fund imetoa msaada wa taulo za kike  zinazoweza kutumika  kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu (reusable pads) kwa zaidi ya wanafunzi wa kike 390 kutoka katika shule za sekondari Ikoma, Sedeko na Manchira.

Aidha, kwa upande wake Bi. Sophia Mnandi- mratibu wa ushauri kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) katika kongamano hilo amewataka wasichana kugeuza changamoto za mila na desturi katika jamii kuwa chachu ya kupaza sauti na kupambania ndoto zao.

"Mila na desturi zetu zisikufanye kuharibu wewe unataka kuwa nani, ndoa za utotoni na mimba za mapema zisikufanye ukashindwa  kufikia malengo, tambua unataka kuwa nani kwani usipojua kuchagua utachaguliwa lolote" alisema Sophia

kwa upande wake  mkufunzi kutoka  chuo cha Afya Kisare Mwl.Restuda Murutta amewaasa wanafunzi hao kuzingatia elimu ya afya ya uzazi pamoja na kuzingatia usafi wawapo katika kipindi cha hedhi pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya taulo za like. 

"tusitupe taulo zetu katika vyoo vya maji hii inasababisha kuziba kwa choo pia ni vizuri kuzingatia usafi hasa kuosha via vya uzazi na tusitumie sabuni zenye kemikali kwani ni hatari kwa afya ya uzazi "

Naye miongoni mwa wanafunzi waliopata mafunzo hayo Rehema Hamad  ameishukuru kampuni ya Grumeti Fund kwa namna wanavyowajali na kuwathamini watoto wa kike na kuahidi kuyaweka katika vitendo mafunzo hayo na kusambaza elimu kwa wengine.

Awali kongamano hili lilitanguliwa na kongamano la vijana wa kiume takribani 435 kutoka shule za Sekondari Robanda, Ikoma, pamoja na Sedeko,  ambapo  Bi. Frida Mollel ambaye ni mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii kutoka Grumeti Fund akaweka wazi lengo la kuwakutanisha pamoja vijana wa kiume kuwa ni kutambua changamoto wanazopitia na kujaribu kutafuta majibu ya changamoto hizo kwa pamoja , lakini pia kuwashirikisha katika kampeni ya kumkomboa binti wa kike waweze kusimamamia ndoto zao.

"tumegundua kuwa watoto wa kike duniani kote wamepewa elimu ya kujitambua lakini baade wanakuja kuishi na wanaume ambao hawajapata elimu hiyo, ndipo tukaona umuhimu wa kuwa na makongamo ya vijana wa kiume, lakini pia vijana wakiume nao wanapitia changamoto nyingi ni lazima tuwasikilize na kuwasaidia wavuke, alisema Bi. Frida Mollel 

Naye mgeni rasmi katika kongamano hilo Ndg. Bwenda Ismail Bainga ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti akawataka vijana wa kiume kulipa kipaumbele suala la maadili kwani ndio msingi wa kila kitu katika maisha.

"tangulizeni maadili katika kila Jambo, isifike hatua mzazi akajuta kuwa kwanini alikuzaa wewe hiyo haipendezi hata machoni pa Mungu, kuweni na tabia njema kwani taifa pia linawategemea" alisema Bainga. 

Kwa takribani miaka saba kampuni ya Grumeti Fund imekuwa ikitoa elimu ya kijinsia kwa wanafunzi wa kike na kiume katika shule za sekondari mbalimbali Wilayani Serengeti na Bunda ambapo tangu mwaka 2017 hadi 2023  taasisi hiyo imefanikiwa kutoa elimu ya kijinsia kwa wasichana 9,236 na kutoa taulo za kike kwa kila binti anayeshiriki mafunzo hayo, huku ikifanikiwa kutoa mafunzo kwa wavulana zaidi ya 3,835 tangu mwaka 2021 hadi Sasa 2023 na kutoa zawadi za jezi na mipira  kwa kila shule iliyoshiriki kwenye kongamano.















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post