SERIKALI YABAINISHA MIKAKATI ENDELEVU KWA AJILI YA KUIMARISHA MFUKO WA UDHAMINI WA KUDHIBITI UKIMWI NCHINI.





Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga akifafanua jambo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kilichofanyika Bungeni Dodoma Tarehe 23 Oktoba 2023 ambapo aliwasilisha Taarifa kuhusu Utekelezaji wa Mkakati Endelevu kwa ajili ya kuimarisha mfuko wa udhamini wa Kudhibiti UKIMWI Tanzania (AIDS TRUST FUND – ATF).






Picha Ikionesha baadhi ya wajumbe katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kilichofanyika Bungeni Dodoma Tarehe 26 Oktoba 2023.

NA; MWANDISHI WETU – DODOMA



Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, inaendelea kushauriana na Serikali kuhusu kuwa na chanzo endelevu na cha uhakika cha Mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI nchini.

Hayo yamesemwa mapema leo Tarehe 26 Oktoba 2023 Bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Buange na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga alipowasilisha Taarifa kuhusu Utekelezaji wa Mkakati Endelevu kwa ajili ya kuimarisha mfuko wa udhamini wa Kudhibiti UKIMWI Tanzania (AIDS TRUST FUND – ATF), kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.

Naibu Waziri Nderiananga alisema, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) inafanya mapitio ya Mkakati wa Ukusanyaji wa Rasilimali kwa kuzingatia wakati, mwelekeo na mahitaji ya sasa na kupitia upya vigezo na malengo ili kufanya maboresho kwa kuzingatia Mkakati ulioboreshwa wa kukusanya rasilimali.

Akiongelea suala la kukuza mchango wa sekta binafsi katika mapambano dhidi ya UKIMWI, Naibu Waziri Nderiananga alisema, Tume imeanzisha mfumo wa majadiliano na wadau kupitia vikao ili kujadili uendelevu wa rasilimali za afua za UKIMWI nchini.

“Malengo makuu ya kuanzishwa kwa Mfuko wa ATF ni pamoja na kupunguza utegemenzi wa rasilimali za kufadhili afua za VVU/UKIMWI kutoka nje ya nchi, kuongeza uendelevu wa huduma muhimu za UKIMWI.” Alisisitiza Nderiananga.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali imeendelea kutekeleza sheria kwa kutenga bajeti ya Serikali kila mwaka kwa ajili ya mfuko huo, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali kwa mujibu wa mwongozo wa mfuko.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stansalus Nyongo alisema ni vizuri Serikali ikatenga na kuongeza fedha za kutosha kwa ajili ya Mfuko huo wa UKIMWI na kuendelea kusema kuwa kamati yake ipo tayari kuhamasiha upimaji wa VVU kupitia mabonanza mbalimbali ya michezo yanayofanyika..



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post