SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA MAENDELEO KATIKA KUIMARISHA MIFUMO NA HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII


Mkurugenzi Mkazi wa Pact Tanzania, Dkt. Levina Kikoyo akipokea tuzo ya umahiri kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Mashaka Biteko. Tuzo hii imetolewa na Serikali ya Tanzania kutambua na kupongeza mchango wa Shirika la Pact Tanzania katika kuboresha mifumo na huduma za ustawi wa jamii.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Mashaka Biteko akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii.
Mkurugenzi Mkazi wa Pact Tanzania, Dkt. Levina Kikoyo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii.
Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Anna Hoffman akihutubia washiriki.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano.
Sehemu ya maafisa ustawi wa jamii wakifuatilia kwa karibu uzinduzi wa mkutano wao wa mwaka.


****
Serikali imesema itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa maendeleo ili kuinua ubora wa mifumo na kiwango cha utoaji huduma za ustawi wa jamii nchini. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Mashaka Biteko wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Mwaka wa Kiutendaji wa Maafisa Ustawi wa Jamii nchini. 

Mkutano huo uliwakutanisha pamoja maafisa ustawi, wizara za kisekta, na wadau wa maendeleo wanaojihusisha na afua za ustawi wa jamii.

Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kutathmini mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta ya Ustawi wa Jamii nchini, na kutoa mkakati wa pamoja wa namna ya kutatua changamoto hizo na kuimarisha huduma za ustawi wa jamii kwa wananchi wenye uhitaji.


Dkt. Biteko aliwaasa wataalam na wadau wa ustawi wa jamii kuendelea kuhudumia wahitaji kwa weledi, uzalendo, na kwa kuzingatia miiko ya utoaji huduma. 

Pia, alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia ili kutibu fikra, hisia na mioyo ya wanajamii ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na kukosa msaada. 

"Mkatumie jukwaa la mkutano huu kujadili mikakati madhubuti ya uboreshaji wa huduma za ustawi wa jamii kwa maslahi mapana ya taifa letu",alisema.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima, alipongeza juhudi za Maafisa Ustawi wa Jamii katika kujenga jamii jumuishi na zenye kujali watu wenye mahitaji maalum.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya kazi na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali ya Marekani kupitia miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ACHIEVE unaotekelezwa na Pact pamoja na washirika wake. 

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Anna Hoffman ambaye ni Naibu Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya afya alisisitiza kuwa ushirikiano baina ya Marekani na Tanzania utaendelea kuimarisha mifumo na huduma za ustawi wa jamii yenye kujali misingi ya uwajibikaji, unafuu na urahisi wa upatikanaji wa huduma, na uadilifu.


Akizungumza kwa niaba ya wadau watekelezaji wa afua za ustawi wa jamii, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Pact Tanzania, Dkt. Levina Kikoyo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mradi wa ACHIEVE, alisema, "Dhamira yetu isiyoyumba kwa mifumo imara wa ustawi wa kijamii ni ushahidi wa imani yetu katika jamii ambapo kila mtu ana fursa sawa ya kufanikiwa bila kujali hali zao au utambulisho wao. Dhima hii si tu ni jambo linalofaa kimaadili, bali ni uamuzi wa kimkakati kwa mustakabali wetu kama Taifa. 

Kwetu Pact, tunaelewa kuwa nguvu ya mifumo imara na huduma thabiti ya ustawi wa jamii inahusiana moja kwa moja na maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi. Tunapowekeza katika ustawi wa jamii, tunawekeza katika ustawi wa taifa letu. Ndiyo sababu tunasimama kidete, kuimarisha mifumo ya ustawi wa jamii, na kuwajengea ujuzi wafanyakazi katika sekta ya ustawi wa jamii ili waweze kutoa huduma zinazohitajika na wahitaji."

Toka mwaka 2020, Shirika la Pact Tanzania limekuwa likitekeleza mradi wa ACHIEVE unaofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI (PEPFAR) na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID). 

Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu na serikali kupitia wizara za mbalimbali kama vile Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, na Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, mradi wa ACHIEVE unafanya kazi na halmashauri na asasi za kiraia kutoa huduma za kijamii, kiafya, na kiuchumi moja kwa moja kwa walengwa.

Kupitia mradi huu, fedha za kitanzania zaidi ya bilioni 20 zimetumika katika kuboresha mifumo na kutoa huduma ambazo zimewakifika watu zaidi ya milioni moja wa katika kipindi cha miaka mitatu (Oktoba 2020 – Septemba 2023).

 Fedha hizi zimetumika kuratibu shughuli za ustawi wa jamii na kununua zana muhimu za kuwezesha utoaji wa huduma za ustawi wa jamii katika mamlaka za kitaifa na serikali za mitaa. Zana hizi ni pamoja na kompyuta, mashine za kupiga chapa na kurudufu, viti, meza, makabati ya kutunzia nyaraka, pikipiki, na magari. 

Pia kupitia ushirikiano huu, Pact Tanzania kupitia ACHIEVE wamewezesha uandaaji, uchapaji, urudufu, usambazaji, na uhuishaji wa utekelezaji wa nyaraka mbalimbali za sera, na miongozo ya kimkakati katika kuimarisha mifumo wa ustawi wa jamii. 

Mojawapo ya zana hizi ni Mwongozo wa Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii unaosaidia halmashauri kupanga, kubajeti, na kuweka maswala ya ustawi wa jamii katika bajeti za Halmashauri, yaani CCSWOP. 

Pia, mradi umeendelea kuratibu huduma za ustawi wa jamii na kutoa mafunzo katika ngazi mbalimbali za serikali, ikiwemo uanzishaji wa Kamati za Ulinzi za Wanawake na Watoto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post