DP WORLD : KKKT YAUNGA MKONO UWEKEZAJI, YAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA HEKIMA

 

Arusha, Agosti 21, 2023


Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo, amesema kuwa kanisa lake lina imani na namna ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan analisimamia suala la uwekezaji kwenye bandari na kumpongeza Rais kwa uongozi wake wenye hekima.


Kanisa la KKKT limesema kuwa linamuunga mkono Rais Samia na linaunga mkono uwekezaji nchini.

KKKT pia imekemea watu wanaotaka kuligawa taifa kupitia kwa mjadala unaoendelea wa bandari kwa maslahi yao binafsi ya kidini, kisiasa na kiuchumi.


Zifuatazo ni kauli 10 nzito zilizotolewa na KKKT kupitia kwa Askofu Mkuu Dk Shoo:


1. "Lipo hili la DP World Mheshimiwa (Rais). Kwanza naomba lieleweke wazi kwamba kanisa linaunga mkono uwekezaji. Hatupingi uwekezaji Mheshimiwa Rais"


2. "Tunajua wewe (Rais) kwenye nia yako unataka wawekezaji"


3. "Sisi viongozi wa dini zote kwa uwakilishi tuliomba kuja kukuona pale mwanzoni kabisa mwa jambo hili (mjadala wa DP World) na kwa uungwana wako na kwa unyenyekevu ulionao na utayari wa kusikiliza, ulitupokea na tulikuletea maoni yetu kama taasisi na viongozi wakuu wa dini katika nchi yetu ya Tanzania. Madhehebu yote ya Kikristo, tukiwa CCT, tukiwa TEC na tukiwa BAKWATA. Mimi nakumbuka jinsi ulivyotupokea, ukatusikiliza. Ukapokea maoni yetu na ushauri wetu viongozi wa dini na ukaahidi kuwa maoni na ushauri hayo utayapeleka kwa wataalamu na kufanyiwa kazi kwa uzito kwa maslahi mapana ya taifa"


4. "Tuna imani na wewe Mheshimiwa Rais"


5. "Tunakuamini Mheshimiwa Rais na tunaamini kwamba ukisema taasisi zako na vyombo vyako vitafanyia kazi jambo hili (ushauri wa viongozi wa dini), unamaanisha hivyo"


6. "Katika jambo hili tunaelekea mahali ambapo tunataka kugawanyika kabisa, wengine wanatumia sababu za kidini, wengine wana maslahi yao ya kisiasa na maslahi ya kiuchumi"


7. "Namshukuru Mungu amekujaalia (Rais Samia) hekima katika hili (mjadala wa bandari) kama Mama na Kiongozi, umekaa kimya"


8. "Jambo hili (bandari) linahitaji hekima kubwa la kuliendea na sisi tunaendelea kukuombea (Rais) kwa Mungu ili hekima yote itumike katika kuweza kuleta muafaka wa jambo hili pasipo kutumika kama kitu cha kuchochea wananchi kwa watu wenye malengo yao mengine"


9. "Mheshimiwa Rais kanisa liko pamoja na wewe"


10. "Tutaendelea kukuombea (Rais)  na kukuunga mkono katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yetu kwa maslahi mapana ya nchi yetu"


Dkt Shoo alitoa kauli hizo leo jijini Arusha mbele ya Rais Samia kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya KKKT.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post