MWENGE WA UHURU WAZINDUA MRADI WA MAJI KASHENGE - ILOGERO, WANANCHI WAHAMASISHWA KULINDA VYANZO VYA MAJI

Na Mariam Kagenda - Kagera 

Wananchi wa kata ya Katoma na Karabagaine wilaya ya Bukoba vijijini mkoani Kagera wamehimizwa kuhakikisha wanalinda na kutunza chanzo cha maji Kyeiringisa kwa kutofanya shughuli za kijamii katika chanzo hicho kwani kikikauka wataendelea kupata changamoto ya maji.


Wito huo umetolewa na Meneja wa  Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)  Wilaya ya Bukoba, Mhandisi Evaristo Mgaya baada ya Mwenge wa Uhuru kuzindua mradi wa maji Kashenge –Ilogero uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 768 ambapo mwenge huo umekimbizwa katika halmashauri ya Bukoba vijijini na umetembelea, kuzindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.


Mhandisi Mgaya amesema kuwa chanzo hicho ni kikubwa kwani kinatokea kata ya Karabagaine na kuleta maji Kata ya Katoma hivyo wananchi wa kata hizo wanatakiwa kukitunza ili kitumike kwa vizazi vya sasa na vijavyo kwani mradi wa maji ni chanzo kikishakauka mradi hautokuwa na faida kwa wananchi hao .

Amesema kuwa ili chanzo hicho kiweze kudumu kwa muda mrefu wananchi hawatakiwi kufanya shughuli za kibinadamu katika chanzo hicho ikiwa ni pamoja na kutokuchoma moto na kutolima jirani na chanzo cha maji.


Ameongeza kuwa mradi huo ni mkombozi wa tatizo la upatikanaji wa maji ambalo limewakumba wananchi wa vijiji hivyo kwa muda mrefu sana hivyo ni matarajio ya serikali kuwa mradi huo utakuwa kichocheo cha maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kata ya Katoma wamesema kuwa kuzinduliwa kwa mradi huo kutawasaidia kuepukana na adha waliyokuwa wanapata kwani iliwalazimu kuamka saa kumi za usiku kwenda kuchota maji kwenye vyanzo vya asilia,  maji hayo hayakuwa safi na salama hivyo wanaishukuru serikali kwa kuwakumbuka na kuwajengea mradi huo.


Kwa upande wake kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa Abdalla Shaib Kaim ameendelea kuwasisitiza wananchi kulinda na kuitunza miradi ambayo inajengwa ili kutimiza adhima ya serikali ya kuhakikisha inatatua changamoto ya maji na kumtua mama ndoo kichwani kwani serikali haipendi kuona wananchi wake wanateseka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post