WAZIRI MKENDA:TURUDISHE HUDUMA ZA MAKTABA KATIKA NGAZI ZA WILAYA NA TARAFA

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akisoma  kitabu mara baada ya kutembelea Maktaba ya Taifa  jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameutaka uongozi wa Bodi ya Huduma za Maktaba kutoendelea na ujenzi wa majengo na badala yake wajikite katika ununuzi vitabu mbalimbali vya maktaba.

Prof. Mkenda ametoa agizo hilo Julai 28, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Menejimenti na watumishi wa bodi hiyo ambapo amesema kazi ya bodi hiyo ni kuhakikisha kunakuwa na maktaba zenye vitabu vya kutosha ambavyo vitawezesha watanzania kupata maarifa.

Waziri huyo ameongeza kuwa badala ya bodi hiyo kuwekeza fedha nying kwenye masuala ya ujenzi wa majengo fedha hizo zielekezwe katika kununua vitabu na kuvisambaza katika maktaba nchini ili kuwapa fursa watanzania kujisomea.

" Jukumu la kipaumbele kwenu si majengo, kazi yenu kubwa ni kuhakikisha maktaba zinakuwepo na mnanunua vitabu na vya maktaba hizo ili kutoa fursa kwa wananchi kujisomea" amesisitiza Kiongozi huyo.

Prof. Mkenda amefafanua kuwa Bodi hiyo inaweza kutafuta maeneo katika taasisi zikiwemo shule, vyuo vya maendeleo ya wananchi ama VETA vikatumika kama maktaba ambazo zitakuwa karibu na jamiii.

Ametolea mfano kwamba katika miaka ya nyuma kulikuwa na maktaba ambazo zilisambaa mpaka katika ngazi za tarafa na wala hakukuwa na majengo ya maktaba lakini wananchi waliweza kusoma na kuazima vitabu

" Mimi ni mnufaika wa maktaba hizi nimezaliwa kijijini na kusomea huko lakini kulikuwa na maktaba ambazo tulizitumia kuazima vitabu na kujisomea lakini leo hakuna maktaba kama hizo embu turudi huko, leo tunaongelea maktaba tatu tu za tarafa hapana tujitafakari" amesema Waziri huyo

Mkenda amewataka kuhakikisha Maktaba zinakuwa na vitabu mbalimbali vivyoandijwa na Watanzania waliopo nchini na nje ya nchi vikiwemo vitabu vilivyoandikwa na viongozi mbalimbali.

Mkurugrenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Dkt. Mboni Ruzegea amemwambia waziri kuwa wamepokea maelekezo na kwamba bodi hiyo ina wajibu wa kutoa fursa kwa wananchi kutumia maktaba za umma ili kujipatia elimu, maarifa na taarifa mbalimbali zitakazosaidia kujikwamua katika umasikini, ujinga na kujipatia maendeleo.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji amesema majukumu ya kisheria ya Bodi ni pamoja na kuanzisha, kuongoza, kuendesha, kutunza na kuendeleza maktaba zote za umma nchini kuanzia ngazi za wilaya, mikoa hadi Tarafa lakini pia kuupatia umma wa watanzania taarifa mbalimbali zilizokusanywa kutoka katika ulimwengu mpana wa maarifa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiwa na Mkurugrenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Dkt. Mboni Ruzegea akikagua Ukumbi wa Mikutano wa Maktaba ya Taifa kabla ya kuzungumza  na Menejimenti na watumishi wa bodi hiyo  jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akisoma  kitabu mara baada ya kutembelea Maktaba ya Taifa  jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo,wakiangalia Vitabu kwenye Maktaba ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo,akisoma kitaba kwenye Maktaba ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiteta jambo na  Mkurugrenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Dkt. Mboni Ruzegea mara baada ya kutembelea  Maktaba ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post