WAZIRI GWAJIMA ATOA MAAGIZO KWA FAMILIA KUHUSU MMOMONYOKO WA MAADILI NA UKATILI


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mayamaya, kata ya Zanka, wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma katika kuelekea siku ya kimataifa ya familia itakayoadhimishwa Mei 15, 2023.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akisisitiza jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mayamaya, kata ya Zanka, wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma wakati akizungumza kuelekea siku ya kimataifa ya familia itakayoadhimishwa Mei 15, 2023.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akiwaimbisha watoto wimbo wa "Don't Touch" ili kuwaelimisha kujiepusha kufanyiwa vitendo vya ukatili kuelekea maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Familia, alipotembelea kijiji cha Mayamaya, wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kwa lengo la kuzungumza na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Wananchi wa Kijiji cha Mayamaya wilaya humo, kuelekea Siku ya Kimataifa ya Familia itakayoadhimishwa Mei 15, 2023.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku akieleza jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mayamaya, wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma kuelekea siku ya kimataifa ya Familia itakayoadhimishwa Mei 15, 2023.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti, akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Wananchi wa Kijiji cha Mayamaya wilaya humo, kuelekea Siku ya Kimataifa ya Familia itakayoadhimishwa Mei 15, 2023.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bahi Stewart Masima,akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Wananchi wa Kijiji cha Mayamaya wilaya humo, kuelekea Siku ya Kimataifa ya Familia itakayoadhimishwa Mei 15, 2023.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mayamaya, wilaya ya Bahi, mkoa wa Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (hayupo pichani) alipotoa ujumbe wa siku ya Kimataifa ya Familia itakayoadhimishwa Mei 15, 2023.



Na.Alex Sonna-BAHI

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,amezitaka Familia kuwafuatilia watoto katika masuala ya maadili ili kujiepusha na changamoto ya mmomonyoko wa maadili inayotajwa kukithiri ndani ya jamii katika siku za hivi karibuni.

Dkt.Gwajima ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mayamaya, kata ya Zanka, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Familia itakayofanyika Mei 15, 2023.

Waziri Gwajima amsema kuwa kasi ya kuporomoka kwa maadili inachochewa na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo watoto na vijana wamekuwa wakiiga tamaduni na desturi za jamii zingine zinazokinzana na mila na desturi za mtanzania.

"Maadhimisho haya yanawakumbusha wazazi wote wawili na walezi wajibu wao wa msingi katika malezi ya watoto na familia hasa maeneo makuu matatu ya msingi ambayo ni kumjali mtoto kwa mahitaji ya msingi, kumlinda mtoto dhidi ya ukatili na kuzungumza na mtoto mara kwa mara ili kufahamu changamoto zinazomkabili na kufahamu maendeleo yake kwa ujumla" amesema Dkt. Gwajima.

Hata hivyo Dkt. Gwajima ametaja changamoto za kiuchumi ndani ya familia kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili ambapo wazazi au walezi wamejikuta wakitumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi na kusahau wajibu wao wa kusimamia malezi na makuzi yenye maadili mema kwa watoto.

"Mtoto anaanzishwa kufanyiwa vitendo vya ukatili toka mdogo hadi anakwenda kufundisha na wengine shuleni na mzazi upo, mbona Ng'ombe na mbuzi mnawafuatilia kuliko watoto, Maadili yanatengenezwa kwenye familia, nyumba za ibada, shuleni na vyuoni ili mtoto apite kote akutane na maadili hivyo tumieni muda wenu kuwafatilia watoto " amesema Dkt. Gwajima

Dkt. Gwajima amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhimiza maadili mema na upendo ndani ya familia, bado kuna matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto katika familia, shuleni na kwenye jamii ikiwemo ukatili mitandaoni.

"Taarifa ya Hali ya Ukatili wa Watoto Mtandaoni Tanzania kwa mwaka 2021 inasema, asilimia 67 ya watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17 ni watumiaji wakubwa wa vifaa vya kielektroniki ambavyo ni simu, komputa na runinga ambavyo kwa kiasi kikubwa maudhui yake yanakuwa na viashiria vya maadili yasiyofaa"

Awali Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe amesema wilaya hiyo imeshaanza mikakati ya kukabiliana na suala la mmomonyoko wa maadili kwa kuwaandaa vijana na wameibeba ajenda ya kupinga ukatili kuwa endelevu ambapo mpaka sasa wameshatengeneza klabu za kupinga ukatili katika Shule zote za msingi na sekondari za Wilayani humo

"Tumeshakutana na walimu wakuu wa shule zote, Maafisa elimu kata, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii kuanzia ngazi ya chini mpaka wilaya" amesema Gondwe..

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo uliokwenda sambamba na mashindano ya mpira wa miguu kwa lengo la kutunza mazingira wamesema wazazi wanatakiwa kusimamia watoto wao dhidi ya mazingira hatarishi kwa kuwapa elimu.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Familia Mwaka huu ni "Imarisha Maadili na upendo kwa Familia Imara" na yataadhimishwa kwenye kila mkoa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post