RAS KUSAYA AWAKARIBISHA WADAU WA BIASHARA NDANI NA NJE KUWEKEZA RUKWA




Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Gerald Kusaya amewakaribisha wadau wa biashara wa ndani na nje kuja kuwekeza katika Mkoa huo wenye mazingira mazuri ya biashara. maliasili, madini, nguvu kazi ya kutosha, soko la kutosha, hali nzuri ya hewa na kijiografia ya kuvutia .

Ameyasema hayo wakati akifungua Maonesho ya Kilimo, Viwanda na Biashara Mkoani Rukwa yanayofanyika katika viwanja vya Nelson Mandela Mei 25 hadi 31, 2023 yanayoongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Uhamasishaji wa Uwekezaji katika Kilimo, Viwanda na Biashara unaozingatia uhifadhi wa Mazingira”

Bw. Musabila pia ametoa rai kwa Mkoa huo kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo sambamba na kuondoa vikwazo vyovyote vya uwekezaji na biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje kwa kuwa Mkoa huo una fursa ambazo zikiendelezwa ipasavyo zitaleta tija na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.

Aidha , amesema Serikali imekuwa ikiendeleza Mkoa huo katika miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege, bandari na meli ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Kabwe na Kasanga, ujenzi wa meli za abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika na ukarabati wa Meli ya MV Liemba unaoendelea ili kuufanya Mkoa huu ufunguke kibiashara na uwekezaji na kufikia kwa urahisi masoko ya ndani na nje ya Nchi.

Akitaja fursa za uwekezaji zilipo Mkoani humo, amesema Mkoa wa Rukwa umebarikiwa kuwa na madini ya helium katika maeneo ya bonde la ziwa rukwa ambayo yako katika hatua ya utafiti pamoja na Madini ya Makaa ya Mawe na Vito ambayo uchimbaji wake umeanza kufanyika.

Vile vile Katibu Tawala huyo amesisitiza wajibu wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini kwa kuwaibua na kiwahamasisha wawekezaji wa ndani kuwekeza katika viwanda badala ya shughuli zingine za kibiashara kama vile uchuuzi na utoaji huduma kwa kutumia mitaji waliyonayo

Aidha Katibu Tawala huyo amewashauri wawekezaji hao kuwekeza katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo ili kuyaongezea thamani kwa kuwa Mkoa huo unazalisha mazao mengi ya kilimo hususani Mahindi na Mpunga na umeanza kilimo cha mazao ya Kimkakati ya Korosho, Chikichi na alizeti katika maeneo ya bonde la ziwa rukwa na Ufipa ya Juu.

Naye Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe Charlota Ozaki Macias ametembelea maonesho hayo katika viwanja vya Nelson Mandela na kusema kuwa Mkoa wa Rukwa umebarikiwa sana kuwa na fursa za uwekezaji hasa madini, mvua za uhakika hali inayoruhusu kilimo bora na amewapongeza Kabila la wafipa kwa kuweza kuhifadhi vizuri historia ya kabila hilo la wafipa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments