WIZARA YA ARDHI KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WADAIWA SUGU


Kamishna wa Ardhi msaidizi mkoa wa Dodoma Jabir Singano.
Mkuu wa Kitengo cha kodi wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Denis Masami akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu ukusanyaji wa madeni ya pango la ardhi.


Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

SERIKALI kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema itawafikisha mahakamani watu wote wanaodaiwa malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na kukamata mali zao na kubatilisha hati zao mara baada ya kuisha kwa kipindi cha msamaha wa Rais Aprili 30, 2023.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mkuu wa Kitengo cha kodi wa wizara hiyo Denis Masami,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ukusanyaji wa madeni ya pango la ardhi katika kipindi ambacho serikali ilitoa msamaha kwa wadaiwa kulipa bila riba.

Denis amesema,"Mheshimiwa Rais alitoa msamaha kwa waliolimbikiza malipo ya kodi ya pango la ardhi katika kpindi cha kuanzi mwezi Julai hadi Desemba mwaka jana ambapo watu 6,000 walijitokeza kutumia fursa hiyo na kulipa bila riba.

Cha kushangaza watu wengi waliomba muda uongezwe na serikali kutoa msamaha kwa awamu ya pili ya kuanzia mwezi Machi hadi Aprili mwaka huu, ambapo hadi sasa ni watu 8,725 wamejitokeza kulipa bila riba”,amesema.

Amesema hadi sasa kiasi cha malimbikizo ya kodi ambacho kimeshalipwa ni Sh. bilioni 31.5 na kiasi cha riba ambacho kimesamehewa ni Sh. bilioni 21.3.

“Hivyo basi niwasihi wananchi kutumia fursa hii ya msamaha wa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, kulipa malimbizo ya madeni yao kodi ya pango la ardhi bila riba kwani muda ukifika mwisho wote walishindwa kulipa tutawachukulia hatua ikiwemo kuwafikisha mahakamani na kushikilia mali zao na kubatilisha hati zao”,amesema.

Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi msaidizi mkoa wa Dodoma Jabir Singano, amesema katika kipindi cha msamaha wa Rais watu zaidi ya 1,200 wamejitokeza kulipa madeni yao.

Amefafanua kuwa kwa mkoa wa Dodoma pekee watu zaidi ya 1,200 wamejitokeza kulipa na kiasi cha Sh. bilioni 1.2 kimeshalipwa hadi sasa na kwamba wanaendelea kuhimiza wote ambao bado wanadaiwa kulipa katika muda huu uliobaki.

Amesema katika jitihada za kuongeza makusanyo mkoa umeendelea kutatua kero zilizokuwepo ikiwemo kukwama kwa malipo ya miamala ya maombi ya wateja.

“Lakini pia kulikuwepo na shida ya upatikanaji wa namba za malipo (contral numbar) hili pia tumelifanyia kazi ambapo tumetoa namba za malipo zaidi ya 4,050 kwa wateja kupitia timu yetu tuliyoiunda kulifanyia kazi suala hili lililokuwa kikwazo kwa wananchi wetu”,amesema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post